DIT kutumia Bilioni 74 kuboresha mfumo ufundi sekta ya mawasiliano

16Jan 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
DIT kutumia Bilioni 74 kuboresha mfumo ufundi sekta ya mawasiliano

CHUO  cha Teknolojia cha Dar es salaam (DIT ) kinatarajia kutumia zaidi ya Tsh. Bil.74 kuboresha mafunzo ya ufundi  hususani kwenye sekta ya mawasiliano na ngozi  ili kuendeleza mpango wa serikali wa kukuza uchumi  kupitia viwanda.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho Prof. Maulilio Kipanyula  wakati wa mahafali ya pili ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Kampasi ya Mwanza , yaliyofanyika Jijini hapa.

Alisema mradi huo wa miaka mitano  umelenga kukabiliana na changamoto za ajira kwa  kuboresha mikundombinu  ya kujifunzia na kufundishia na kuleta mageuzi makubwa hasa kwenye miundombinu ya kufundishia .

Alisema  DIT itapata Billion 74 kwa ajili ya mradi unaolenga kuboresha mafunzo ya ufundi yanayohitajika katika soko la ajira katika kanda ya Afrika Mashariki (EASTRIP) ambao kwa kiasi kikubwa mradi huo umejikita kuendeleza miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

“Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB). Inatarajiwa kuwa baada ya ufadhili huo, DIT itatambulika kikanda kwa umahiri katika uendeshaji wa mafunzo ya Tehama na ngozi,” alisema Professa Kipanyula.

Aliongeza kuwa baada ya kutekelezwa kwa mradi huo Taasisi ya DIT katika eneo la Afrika Mashariki itakuwa ndio kituo mahiri katika teknolojia ya habari , mawasiliano na ngozi .

Aidha alisema wana mradi mwingine wenye thamani ya kwa Euro 11.7 milioni sawa na Sh33 bilioni ambao ni wapili wa kuendeleza ajira na elimu ya ufundi hapa nchini (TELMS II) ambao una lenga kuisaidia Taasisi hiyo  kujitegemea na kuendesha mafunzo ya ufundi kwa ufanisi zaidi ili kuzalisha wataalamu wanaoajirika au wanaoweza kujiajiri ambao unafadhiliwa na Serikali ya Italia.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo imejipanga kuchochea maendeleo ya viwanda nchini, kwa kuweka utaratibu wa kutambua na kuendeleza teknolojia na ubunifu unaofanywa na wanafunzi na watumishi wa Taasisi kwa kuanzisha atamizi na Kampuni ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT Co. Ltd).

Naye Mkuu wa DIT, Professa Preksedis Ndomba alisema katika mahafali hayo wamehitimu wanafunzi 18, katika ngazi ya Stashahada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara ambapo mfumo wa utoaji mafunzo ulikuwa ni muda mwingi kwenye vitendo na ziara kwenye maabara na viwanda.

Alisema mfumo huu umezalisha wataalam waliobobea katika ufundi, ubunifu na ujasiriamali ili kuwawezesha kujiajiri, mkakati unaoendana na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17 na 2020/21 na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Emmanuel Kapole akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alisema  jamii ina matumaini makubwa na elimu waliyoipata hivyo imani yake wataitumia  kutatua changamoto zinazowakabili sambamba na kuitumia kwa manufaa binafsi,familia na taifa.

Alisema serikali imelenga kuanzisha viwanda vidogovidogo  vyakati na vikubwa na kuvifufua viwanda ambavyo kwa sasa havina ufanisi, lengo la makuzi hayo ni kuongeza thamani kwenye bidhaa mbalimbali ambazo zinauzwa nje ya nchi zikiwa ghafi hivyo wanahitaji kuziboresha ili zisiuzwe ghafi na kuwa bidhaa zilizoongezwa thamani .

Alingeza kuwa kwa kulifanikisha ili serikali itakuwa imetenengeneza ajira kwa wahitimu wote wa vyuo na kimarisha uchumi wanchi na kupiga vita umaskini kwa kuweka mazingira mazuri kwa wahitimu wa elimu ya juu.

Habari Kubwa