KUELEKEA UCHAGUZI MITAA: CCM yawataja Mbowe, Zitto

25Jun 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
KUELEKEA UCHAGUZI MITAA: CCM yawataja Mbowe, Zitto

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina uhakika wa kushinda kwa asilimia 95 uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, huku kikitamba kuwa katika Uchaguzi Mkuu mwakani, kitachukua majimbo ya Hai na Kigoma Mjini yanayoongozwa na wabunge Freeman Mbowe na Zitto Kabwe, mtawalia.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ccm, Humphrey Polepole.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alipozungumza na waandishi wa habari.

Polepole alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu katika halmashauri zote 185, chama hicho hakitakubali kumpitisha mtu yeyote kugombea kama hajafanya kazi ya kuhudumia wananchi.

Alisema viongozi wote watakaopitishwa na chama hicho kugombea katika uchaguzi huo ni wale tu wenye shughuli za kufanya kwa ajili ya kujiingizia kipato, waliofanya kazi ya kutoa huduma bora kwa wananchi na wenye sifa stahiki.

“Viongozi wote ambao hawakuwajibika kuhudumia wananchi na kushughulika na utatuzi wa kero zao, wasipewe nafasi katika uteuzi wa serikali za mitaa.

"Chama kimeshatoa mwelekeo kwamba viongozi wanaotakiwa kuchaguliwa ni wachapakazi, wenye kazi inayowaingizia kipato, waadilifu, waaminifu, wanyenyekevu, wanaochukizwa na rushwa, wanaojishusha, wazalendo kweli na wakali kwa mambo ya ovyo.

“CCM mpaka sasa ina wanachama zaidi ya milioni 15, na wapigakura wa Tanzania ni milioni 21. Kwa hiyo, tukipiga hesabu kwa wanachama pekee, tunapata kura asilimia 71 ya ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao. Na tukifanya kampeni kuzunguka katika mikoa yote, tunapata kura zaidi ya asilimia 90," Polepole alisema.

Kiongozi huyo alisema Kamati Kuu ya chama hicho inatarajiwa kukutana leo na makatibu wa chama hicho kutoka mikoa yote na kesho inatarajiwa kufanya kikao chake kikiongozwa na Mwenyekiti, Dk. John Magufuli na keshokutwa itatembelea miradi mbalimbali.

MBOWE, ZITTO

Polepole alisema anaamini CCM mwakani itaibuka na ushindi katika majimbo mengi ambayo sasa yanaongozwa na upinzani, yakiwamo Hai na Kigoma Mjini ambayo Mbowe na Zitto wanayashikilia.

Alidai Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekuwa kikiwaaminisha Watanzania kwamba mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ni ngome yake, lakini anaamini dhana hiyo itafutika mwakani.

Polepole alidai kufanya vizuri kwa Chadema katika mikoa hiyo kulitokana na kutoelewana kwa wanachama na viongozi wa CCM katika maeneo hayo.

Alidai kutokana na kumalizika kwa tofauti hizo kulikokwenda sambamba na kurejea kwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, hakuna jimbo hata moja katika uchaguzi ujao ambalo litakwenda upinzani kwenye mikoa hiyo.

Alidai Mbowe amekuwa akipiga kelele kwamba vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara wakati hata katika jimbo lake lenyewe haendi kufanya mikutano hiyo.

“Chama cha Mbowe kimeanza kusema kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha daftari la wapigakura katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ili kuwanyima haki wapigakura katika mikoa hiyo kwa sababu ni ngome ya Mbowe, nani kakwambia Arusha na Kilimanjaro ni ya Mbowe?" Polepole alihoji.

“Na kinachotaka kuwaaminisha ionekane kwamba kule kulikuwa ni ngome ya Chadema, kulitokana na tofauti zilizotokea kwa baadhi ya wanachama wetu kuhama ambao hata hivyo tayari wamesharudi.

"Upinzani umeingia Kilimanjaro na Arusha kutokana na tofauti zilizotokea ambazo hata walioongoza tofauti hizo tayari wamerudi akiwamo mzee wetu mstaafu. Kwa hiyo, mikoa hiyo haijawahi kuwa ngome ya upinzani na mimi nataka kuwaambia kuwa 2020 hakuna atakayebaki huko."

Polepole pia alimtumia salamu Zitto, akidai naye ajiandae kuondoka katika jimbo lake kwa kuwa amekuwa akitoa taarifa alizodai za uongo.

“Unawezaje kusema uchumi umeporomoka wakati serikali inaendesha miradi yake na kufanya mambo makubwa ya maendeleo ikiwamo kununua ndege, kutengeneza barabara, reli na mengine kwa kutumia pesa yake ya ndani?

"Tunamtaka huyu ndugu yetu Zitto atafute kazi ya kufanya badala ya kuendelea kuwadanganya wananchi. Na tulishamwambia kwamba katika jimbo lake lile ajiande kutafuta kazi nyingine kwa sababu 2020 harudi," Polepole alitamba.

Habari Kubwa