Mkwasa apigia hesabu tatu za Yanga Ligi Kuu

14Jun 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mkwasa apigia hesabu tatu za Yanga Ligi Kuu

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwassa, amesema tayari kikosi chake kimerejea kambini na kuanza mazoezi kwa ajili ya kuivutia kasi Yanga katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwassa.

Akizungumza na gazeti wiki iliyopita, Mkwassa alisema hawako katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo, hivyo analazimika kuiandaa timu yake vizuri kwa ajili ya kutafuta pointi tatu katika kila mechi iliyopo mbele yao ikiwamo dhidi ya Yanga watakayocheza Alhamisi wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alisema anaamini utakuwa mchezo mgumu na wa ushindani mkubwa kwa sababu kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo.

“Mechi nyingi hivi karibuni hatukufanya vizuri, sasa tunajipanga kuanza na dhidi ya Yanga, Polisi Tanzania na Namungo FC, hizo tunahitaji kupata pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kubaki katika Ligi Kuu.

“Kwa sasa hakuna kubeza timu yoyote, tutakosa baadhi ya wachezaji kuelekea mchezo wetu dhidi ya Yanga, kutokana na kutumikia adhabu ya kadi na majeruhi, lakini tayari nimewaandaa vijana wangu kuhakikisha wanapambana kufikia malengo yetu,” alisema Mkwassa ambaye timu yake inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 37.

Habari Kubwa