JPM aanika walichoteta dakika za mwisho na Mkapa

29Jul 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
JPM aanika walichoteta dakika za mwisho na Mkapa

RAIS John Magufuli ameeleza alivyozungumza na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, na kumpa maneno ya mwisho saa chache kabla ya kifo chake.

Mkapa (1938-2020), alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa hospitalini jijini Dar es Salaam kutokana na shambulio la moyo.

Katika hotuba yake jana wakati wa kuaga mwili wa Mkapa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini na baadaye kusafirishwa kwenda kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara kwa mazishi yatakayofanyika leo mchana, Rais Magufuli alifunguka walichoteta na kiongozi huyo.

Rais Magufuli alisema alipata fursa ya kuzungumza naye saa chache kabla ya umauti kumfika, akisema: “Binafsi nilipata fursa ya kuongea na Mzee Mkapa kwa njia ya simu akiwa hospitalini saa chache kabla hajafariki (dunia).

"Ninakumbuka wakati nikiongea naye, aliniambia 'John usiwe na wasiwasi, ninaendelea vizuri'. Sikujua kwamba maneno yale yalikuwa ya kuniaga, Ninamshukuru Mungu kwa zawadi ya Mzee Mkapa, kazi ameikamilisha,"

Rais Magufuli alisema kwa hisia kali huku akifuta machozi. Rais Magufuli alihitimisha hotuba yake akimnukuu mwandishi nguli wa vitabu duniani, Robin Sharm, aliyewahi kusema "When you were born, you cried and the world rejoiced.

Live your life so that when you die, the world cries and you rejoice." Tafsiri yake ikiwa ni “Wakati unazaliwa ulilia, wakati watu waliokuzunguka wakifurahi. Kwa hiyo, unatakiwa uishi vizuri ili siku ukifariki dunia, ufurahi wakati watu wengine wanaokuzunguka wakulilie."

Rais Magufuli alisema kutokana na umati huo uliojitokeza tangu walipoanza kuaga mwili huo Jumapili na wageni waliofika nchini pamoja na salamu nyingi kutoka mataifa mbalimbali akiwamo Papa wa Kanisa Katolika, hakuna shaka Mzee Mkapa aliishi maisha yake vizuri.

“Vitabu vya dini vitatueleza, tujitahidi kutenda mema duniani ili tutakapoondoka tutavikwa taji,” alisema.

Aliwashukuru Watanzania kwa kuwa watulivu tangu msiba ulipotokea na kuungana kwa pamoja katika kuomboleza.

Alishukuru taasisi za dini kupitia viongozi wake kwa kuendelea kuiombea familia ya Mkapa hasa mke wake, Mama Anna Mkapa, huku akivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia amani na utulivu pamoja na vyombo vya habari kwa kuhabarisha umma kuhusu yote yanayotokea kwenye msiba huo.

Habari Kubwa