ACT yatoa msimamo Membe kuwania urais

23May 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
ACT yatoa msimamo Membe kuwania urais

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimebainisha msimamo kuhusu uwezekano wa kumpa nafasi ya kuwa mgombea wake wa urais, aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benard Membe.

aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benard Membe. picha mtandao

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema ikitokea kada huyo akajiunga na chama hicho na kutimiza vigezo vinavyotakiwa, anaweza kupewa nafasi hiyo.

Alisema ACT-Wazalendo inatambua kile alichokiita kutotendewa haki kwa baadhi ya wanachama wa chama tawala, CCM wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.

“Tuna imani kwamba baadhi ya watu watataka ‘kum-challenge’ (kuchuana na) Rais John Magufuli, kwa mfano tumemsikia ndugu Membe ambaye amefukuzwa uanachama. Lakini, kwa taarifa zilizopo ni kwamba anaendelea kutetea uanachama wake.

“Sasa kwa mfano akigombea, 'I am trying to build a scenario' (ninajaribu kutengeneza hoja) na akashindwa harakati hizo ndani ya CCM, akija ACT kugombea hatuwezi kumzuia, mradi akitimiza sifa za kufanya hivyo.

“Hakuna kikwazo chochote kwa mtu ambaye atakuwa amekatwa katika michakato ya urais, ubunge na udiwani kutoka katika chama kingine kuja kugombea katika ACT-Wazalendo, taratibu zetu zinasema mtu atatangaza nia, atachukua fomu na atashindana.

“Ukishakuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo, unapimwa katika usawa na wanachama wengine, hakuna mwanachama wa miaka sita na mwanachama wa wiki mbili, wote wanapimwa kuwa ni wanachama sawa isipokuwa tutajitahidi kuwa makini kwa uzoefu tulioupata kutoka nyuma kwa maana ya kuangalia rekodi za wahusika.

“(Tunaangalia) nini kimewatoa katika chama husika na chama chetu kinaweza kuathirika vipi iwapo kikimpa nafasi mtu huyo kwenye nafasi fulani.

Tutakuwa na uchunguzi wa kina zaidi kuliko ilivyokuwa 2015 kwa sababu katika miaka hii mitano, kumekuwa na matukio ambayo yamebomoa sana imani ya watu katika siasa za vyama vingi," alifafanua.

Membe (66), aliingia katika mgogoro na chama chake baada ya sauti inayodaiwa ya Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuvuja katika mitandao ya kijamii akiikosoa serikali.

Aliitwa na kuhojiwa na kamati ya maadili ya chama hicho pamoja na makada wengine na waliowahi kuwa viongozi wa juu wa chama hicho; Kanali mstaafu Abdulrahaman Kinana na Yusuph Makamba, waliowahi kuwa makatibu wakuu wa chama hicho.

Februari 28 mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM iliazimia Membe kufutwa uanachama wa chama hicho kwa kile kilichoelezwa na Katibu Mwenezi, Humphrey Polepole, kuwa amekuwa na mwenendo usiofaa tangu 2014 na amewahi kupewa adhabu mbalimbali ambazo hazijasaidia kumbadilisha.

Habari Kubwa