Blockbonds, Benki I & M wazindua huduma

19Feb 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Blockbonds, Benki I & M wazindua huduma

KATIKA kuwezesha Watanzania wengi kumiliki akaunti binafsi na akaunti za biashara, Kampuni ya Blockbonds kwa kushirikiana na Benki I & M imezindua huduma ya Spenn inayomwezesha mtumiaji kutuma na kupokea fedha bila makato yoyote.

Huduma hiyo inayopatikana kwa kuwa na simu janja maarufu smartphone, itamwezesha mtumiaji kujisajili kwa kutumia kitambulisho cha taifa kabla ya kuanza kupata huduma kwa usalama na uhakika.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Blockbonds na Spenn, Jens Glaso, aliyaeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam jana.

Alisema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya huduma za kifedha kupitia teknolojia yenye ubunifu wa hali ya juu.

“Huduma imeanza kupatikana Tanzania na nchi za Afrika, mwaka jana tuliweza kuizindua nchini Rwanda na tayari kuna watumiaji zaidi ya 130,000 ambao wameshajiunga,” alisema Glaso.

Alisema mtu yoyote anaweza kufungua akaunti ambayo haina gharama za uendeshaji na kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo katika maduka mbalimbali pamoja na kuweka na kutoa fedha katika tawi lolote la benki I&M.

Alieleza zaidi kuwa, huduma hiyo pia ina fursa ya kufanya biashara ya kuuza bidhaa na huduma kwa ufanisi kwa kumpa mtumiaji njia rahisi ya kupokea malipo bila kutumia fedha taslimu endapo atajisajili kuwa mtumiaji.

“Ni rahisi sana mtu yoyote anayemiliki simu aina ya smartphone, anaweza kujisajili na Spenn kwa urahisi, na ili kujisajili unapaswa kuwa na namba ya simu, jina kamili pamoja na kitambulisho cha taifa,” alisema Glaso.

Pia, alisema lengo ni kuwafikia mamilioni ya Watanzania ambao hawana akaunti kwa ajili ya kujiwekea akiba kwa njia rahisi na isiyo na gharama.

Habari Kubwa