Bunge lamthibitisha Dk. Mpango kuwa Makamu wa Rais

30Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bunge lamthibitisha Dk. Mpango kuwa Makamu wa Rais

Bunge limemthibitisha Dk. Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania baada ya kupigiwa kura na wabunge wote 363 sawa na asilimia 100.

Akizungumza bungeni leo, spika Job Ndugai amesema wabunge wamepiga kura ya ndiyo kwa Dk. Mpango kuwa Makamu wa Rais baada ya jina kupendekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akiwashukuru wabunge wote kwa kura za ndiyo Dk. Mpango amesema lengo kubwa ambalo atalifanyia kazi ni pamoja na kusimamia uwajibikaji ndani ya serikali.

“Jina langu limeletwa kwenu kwa pendekezo la Rais kwa ajili ya kazi hiyo ngumu ya kumsaidia yeye kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu".

"Nataka niseme kwamba alipofariki Dk John Magufuli nililia sana hadharani lakini pia hata binafsi huko nyumbani lakini baadaye machozi yangu yalikauka kwa sababu Tanzania lazima iendelee.”

“Ningependa sana tutoke kuwa nchi yenye kipato cha chini na kuwa nchi yenye kipato cha juu katika kipindi kifupi na anawezekana kwa pamoja tukiamua kama Watanzania,” amesema Dk. Mpango.

Habari Kubwa