Jacob aahidi hospitali Ubungo

25Oct 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Jacob aahidi hospitali Ubungo

MGOMBEA Ubunge wa Ubungo, Boniface Jacob, ameahidi kujenga Hospitali ya Wilaya ya Ubungo akipewa ridhaa ya kuliwakilisha bungeni, ili kusaidia kuboresha huduma za afya wilayani huko.

Katika mkutano wake wa kampeni Kata ya Kimara jijini Dar es Salaam juzi, Jacob alisema ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo uliokuwa unaendelea katika eneo la Kimara Baruti, ulisimama alipoondolewa katika nafasi ya Meya wa Manispaa ya Ubungo mwaka jana.

“Wananchi wa Ubungo mnajua 'figisu' nilizofanyiwa nikaondolewa katika nafasi ya meya, tangu wakati huo ujenzi wa hospitali ya wilaya ambao msingi ulikuwa umeshawekwa umesimama," alisema.

Mgombea huyo alisema kwa sasa wananchi wa jimbo hilo wanatumia Kituo cha Afya Sinza kama hospitali na kiko mbali na maeneo mengine ya jimbo hilo, hivyo kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Alisema hakumalizia ngwe yake ya uongozi baada ya kufanyiwa kile alichokiita hujuma, lakini alijitahidi kutekeleza ahadi zake zote na kuwaahidi wananchi wa Ubungo kufanya kazi zaidi akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani umepagwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, siku tatu zijazo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeshatangaza kuwapo vituo vya kupigia kura 80,155, Watanzania 29,188,347 wenye sifa, wakitarajia kuchagua wabunge 390 na madiwani 5,350.

Habari Kubwa