CHADEMA yahoji zinakotengenezwa fomu za kupiga kura

11Oct 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
CHADEMA yahoji zinakotengenezwa fomu za kupiga kura

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ijitokeze hadharani na kutaja kampuni iliyoshinda zabuni ya kuchapisha karatasi za kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Hata hivyo, tume hiyo kupitia kwa Mkurugenzi wake, Dk. Wilson Charles, imesema ilishatangaza zabuni hiyo kwenye mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya kieletroniki, hivyo kuwataka CHADEMA waangalie huko kuijua kampuni iliyoshinda.

Jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Juni 30, mwaka huu, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, alisema tume itasema kampuni iliyoshinda zabuni hiyo iliyotangazwa Machi 9, mwaka huu.

“Machi 9, NEC ilitangaza kwenye vyombo vya habari zabuni ya kuitisha kampuni za kuchapisha karatasi za kupigia kura. Taratibu za ununuzi zinataka baada ya kuitisha, ilitakiwa kutoa taarifa kuhusu kampuni gani zilishindanishwa na iliyoteuliwa kuchapisha karatasi hizo,” Mnyika alisema.

Kiongozi huyo wa chama alisema tangu kipindi hicho, ni karibu miezi minne tume haijatangaza kampuni ilishinda zabuni hiyo.

“Hata kamati ya zabuni ya ununuzi inayohusisha vyama vya siasa katika kikao chake cha tarehe nane mwezi huu (Oktoba 8, 2020), hakijaelezwa na NEC jina la kampuni iliyopewa kazi hii,” alisema.

Mnyika alidai kuwa, kupitia vyanzo vyao, wamebaini ipo kampuni ya Tanzania iliyopewa zabuni hiyo wakati awali ilitajwa kampuni ya Afrika Kusini.

“NEC ieleze ni kampuni gani iliyopewa kazi ya kuchapisha karatasi za kupigia kura kati ya hizi mbili; ya Tanzania au Afrika Kusini. Iwapo imebadili mchapishaji, ieleze ni mchakato gani wa ununuzi ulipitiwa kwenye kuteua kampuni ya kuchapisha karatasi hizi," Mnyika alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema endapo ikithibitisha kampuni iliyoteuliwa ni ya Tanzania, NEC itapaswa kuwahakikisha Watanzania usalama wa karatasi hizo.

“Mchapisha karatasi za kura asipokuwa mtu salama mwenye kuaminika na taasisi huru, upo uwezekano wa kuchapishwa karatasi za ziada. Ili uchaguzi usiwe wa hujuma, tume ijitokeze hadharani ieleze ni kampuni gani iliyopewa zabuni,” alisisitiza.

Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia hoja hizo za CHADEMA, Dk. Charles, alisema NEC haijatangaza hadharani kampuni iliyoshinda kwa sababu zabuni ilitangazwa kwenye mfumo na kampuni zilizoomba, nyingi ni za nje.

“Wasitake kuleta taharuki za uongo, waangalie kwenye mfumo tulitangaza, wanajua na zilizoshinda mfumo unaonyesha,” alisema mkurugenzi huyo na kusisitiza kampuni zilizoomba zilifuata utaratibu.

“Waambie tulitangaza kwenye mfumo na zilikuwa ni zabuni za kimataifa, walioshinda wanajulikana, wapo kwenye mfumo, hayo wanasema uongo, muda wa kampeni utaisha mambo yote ya uongo uongo yataisha, watabaki wametulia,” alisema.

Awali, Mnyika alitaka kabla ya mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhusu mfumo wa ujumlishaji matokeo kufanyika, NEC itoe fursa kwa vyama vya siasa kuuona kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, suala hilo lilizua sintofahamu.

“Tushirikishwe kuuona mfumo na wataalamu wetu wa IT waukague kabla haujaanza kufundishwa kwa hao wasimamizi wa uchaguzi,” Mnyika alishauri.

Habari Kubwa