Chadema yaiandikia barua Takukuru

02Jul 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Chadema yaiandikia barua Takukuru

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeindikia barua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kikitoa masharti 6 ya mambo wanayotaka yazingatiwe ili kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ikiwemo kuelezwa makosa yanayochunguzwa na ukomo wa uchunguzi huo.

KATIBU MKUU WA CHADEMA, JOHN MNYIKA: PICHA NA MTANDAO

Akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam ,Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amedai kuwa taasisi hiyo inafanya kazi kwa malengo ya kisiasa kwa kile alichodai kuwa  inakichunguza chama hicho ili kutafuta makosa badala ya kuchunguza kosa.

“Hadi sasa Chadema imeshatoa nyaraka nyingi pamoja na mahojiano mbalimbali ,yanayohusu fedha za michango ya wabunge lakini katika malengo ambayo hayajaelezwa lakini ghafla tunaona tumeandikiwa barua nyingine kwa mambo ambayo hayahusiani” amesema Mnyika

Katibu Mkuu huyo wa Chadema amedai kuwa barua ya Takukuru haijaeleza ni makosa yapi wanayochunguza katika chama hicho wala ukomo wa uchunguzi huo na badala yake kumtaka kiongozi huyo kueleza mambo ambayo ana ufahamu nayo  jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Amesema kuwa Takukuru ilitaka kupata nyaraka mbalimbali ikiwemo taarifa ya hesabu za serikali zilizokaguliwa za miaka ya fedha 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018, 2018/2019 miongozo na kanuni za chama inayotoa idhini ya kukata fedha wabunge pamoja na  nyaraka na stakabadhi za chadema kupokea makato ya wabunge hao.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo watu 60 wakiwemo wabunge wa chama hicho na waliokihama chama hicho pamoja na wanachama mbalimbali wamekwisha fanyiwa mahojiano na taasisi hiyo.

Habari Kubwa