DC Longido atoa angalizo viongozi wa mitaa

13Jan 2020
Zanura Mollel
Longido
Nipashe
DC Longido atoa angalizo viongozi wa mitaa

MKUU Wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe, amewataka wenyeviti na watendaji wa vijiji vilivyo mipakani kudhibiti biashara za magendo zinazotoka na zinazoingia nchini kutoka Kenya kwa kupitia mpaka wa Namanga ulioko mkoani Arusha.

MKUU Wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe, AKIZUNGUMZA NA WENYEVITI WA VIJIJI NAMNA YA KUDHIBITI BIASHARA ZA MAGENDO. PICHA ZANURA MOLLEL

Mwaisumbe ametoa kauli hiyo, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo viongozi hao iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo la Longindo Dk. Steaven Kiruswa iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

"Wakati mwingine mimi na katibu tawala Toba Nguvila hatulali tunapambana kudhibiti magendo yanayopita njia zisizo rasmi na tunazikamata, lakini hamtupi ushirikiano," amesema Mwaisumbe.

Mwaisumbe ameeleza kuwa biashara nyingi za magendo hazipiti barabarani, bali zinapitishwa katika njia zisizo rasmi (panya road), hali ambayo ni hatari kwa Watanzania kwa sababu bidhaa hizo zinawafikia watumiaji wengi tofauti na wachache wanaozivusha.

"Magendo yakiingia nchini ni hatahari kwa taifa na wananchi wake, nendeni mkawe mabalozi wazuri wa kukemea biashara ya magendo kwani yanapita katika maeneo yenu," amesema.

Aidha, amesema kuwa anajiandaa kufanya ziara ya vijiji vyote vilivyopakana na nchi jirani ya Kenya yenye lengo la kuangalia hali ya usalama kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu kwa wananchi waliowapa dhamana.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema ngamia zaidi ya 200, walikamatwa katika kijiji cha Kimokuwa walipokuwa wanafungwa na raia wawili wenye asili ya Kisomali kinyume na sheria za nchi na walifikishwa mahakamani na kutoa faini pamoja na kutakiwa kurudi nchini kwao Somalia.

Habari Kubwa