Dk. Mwinyi: Najiandaa kushona suti ya ushindi

22Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
PEMBA
Nipashe
Dk. Mwinyi: Najiandaa kushona suti ya ushindi

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ana uhakika wa kushinda nafasi hiyo na kwamba kwa sasa anajiandaa kushona suti ya ushindi.

Akihutubia mkutano wa kampeni jana katika Kijiji cha Kiwani, Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba, Dk. Mwinyi alisema ari ya vijana kuiunga mkono CCM ni dalili kubwa ya kupata ushindi wa kishindo.

Dk. Mwinyi alisema kutokana na vijana wengi ambao ni asilimia kubwa ya wapigakura kumuunga mkono yeye ambaye ni mgombea kijana kuliko wote katika kinyang’anyiro hicho, ana kila sababu ya kushona suti ya ushindi.

"Nataka niwaulize kati ya kijana na mzee mtamchagua nani?” Aliuliza Dk. Mwinyi huku umati uliofika kwenye mkutano huo ukijibu: “Tutamchagua kijana.”

Mgombea huyo wa urais alisema kwamba zama za sasa ni za vijana, hivyo akishinda  Zanzibar atatoa nafasi kubwa kwa vijana.

Dk. Mwinyi, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 54, anapambana na Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT- Wazalendo ambaye ana umri wa miaka 77.   

Kuhusu amani, Dk. Mwinyi alisisitiza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kulinda na kudunisha amani kwa kuwa ndiyo nguzo muhimu kwa maendeleo. Alisema bila amani hakuna shughuli zozote za maendeleo zinazoweza kufanyika.

Sambamba na amani, aliwataka wana CCM kudumisha Muungano kwa sababu umewaweka karibu na umekuwa na manufaa makubwa kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na umati wa wana CCM katika Jimbo la Kiwani na maeneo mengine ya kisiwani Pemba. Kufikia saa tano asubuhi uwanja ulisheheni wanachama wa CCM na wananchi waliofika kusikiliza ilani,  sera na mwelekeo wenye kuleta matumaini kwa wananchi.

SHEIN AONYA

Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwaonya wale wote wanaochezea amani, waache kufanya hivyo, vinginevyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Wasiwatishe watu, nguvu na uwezo wa kuwadhibiti tunao na tunawaambia tutailinda amani yetu kwa gharama yeyote ile. Wananchi nataka kuwaambia hakuna wa kukutisheni, tembeeni kifua mbele na siku ya uchaguzi nendeni kwa uhuru na mapana kwenda kupiga kura,” alisema.

“Tumo katika vuguvugu za kampeni za uchaguzi mkuu. Wasitake kutisha watu na wala hawana uwezo huo. Wasione simba kajikunyata wakadhani paka, nawaambia simba si paka. Wasijaribu,” alisisitiza.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuipenda CCM, huku akisema chama hicho kitashinda uchaguzi na kwamba hilo halina mjadala.

“Nasema leo (jana) nikiwa Kiwani, tutawashinda tena ushindi mkubwa. Mwaka huu tutapata ushindi mkubwa sana. Tarehe 28 twendeni tukamchague mgombea wetu Dk. Hussein Mwinyi.

“Dk. Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kujieleza, ana sifa ya kuwa mwadilifu, muungwana, mzalendo wa nchi hii na hana papara. Hana vishindo na huyu ndiyo mwenye sifa za kuongoza Zanzibar. Katika sifa 14 za CCM, anazo yeye ndiyo maana kachaguliwa kuwa mgombea,” alisema.

Habari Kubwa