Elimu, chanjo corona makanisani, misikitini

04Oct 2021
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Elimu, chanjo corona makanisani, misikitini

SERIKALI imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu ya umuhimu wa kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa waumini kanisani na misikini baada ya ibada.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, alibainisha hayo jijini Dodoma alipokuwa akitoa elimu ya umuhimu wa kuchanja chanjo hiyo kwa watumishi wa Wizara ya Madini.

Prof. Makubi alisema kutokana na utoaji wa elimu ambao unafanywa hivi sasa na wizara yake mwitikio wa watu kuchanja umeongezeka kwa kasi.

“Awali Rais Samia alipozindua chanjo hii, idadi ya watu ilikuwa kwa siku watu wanaochanja ni 20,000, lakini baada ya maneno yale yaliyotokea kwenye mitandao ulishuka hadi kufikia watu 1,000 kwa siku. Lakini hivi sasa baada ya kuanzia kampeni hii ya elimu, idadi imepanda hadi watu 30,000 kuchanja kwa siku,” alisema Prof. Makubi.

Alisema hivi sasa wizara yake imezungumza na viongozi wa dini wa makanisa na misikiti mbalimbali nchini ili kuanza kutoa elimu kwa waumini wao kila baada ya ibada kuisha na kutoa chanjo katika eneo husika.

Pia alisema lengo la elimu hiyo ni kuhakikisha kuwa idadi ya watu wanaochanja kwa hiari chanjo ya UVIKO-19 inaongezeka zaidi ya sasa.

Aliwataka Watanzania kuwapuuza watu ambao wamekuwa wakitoa kejeli kuhusu chanjo na kupotosha umma.

“Ndugu zangu, chanjo hizi ni salama kabisa tumefanyia vipimo mbalimbali katika mamlaka zetu na kujiridhisha kuwa ni salama, hivyo msidanganyike na watu hata Hayati Rais Magufuli hakuwahi kusema watu wasichanje, lakini alisema kuwa kama zitakuja inabidi tujiridhishe na ndicho wizara tulisisitiza na kimefanyika,” alisema Prof. Makubi.

Vilevile, alisema chanjo hiyo inayotolewa nchini ni salama na inafaa kwa watu wote wakiwamo wenye magonjwa ya kisukari, kansa, figo, shinikizo la damu na hata mama mjamzito ni ruksa kuchanja.

“Kuna watu wanapotosha kuwa eti mwanamke akichanja anaweza asipate ujauzito kabisa, jambo hili siyo kweli kabisa hakuna mahusiano kati ya chanjo hii na mtu kutopata ujauzito,” alisema Prof. Makubi.

Kadhalika, alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia chanjo hiyo ambayo inaelekea kuisha kabla ya kuingizwa nyingine.

“Ndugu zangu tuchangamkie chanjo hii ambayo hivi sasa mtu anachanja mara moja tuu, hiyo nyingine ikija mtu atalazimika kuchanja mara mbili,” alifafanua.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, aliishukuru Wizara ya Afya kwa kutoa elimu kwa watumishi wake ili kuhamasika kuchanja chanjo hiyo na kujikinga na UVIKO-19.

“Pamoja na elimu hii, lakini hapa tulipo yapo maeneo maalum kwa ajili ya kutoa chanjo… mimi nilishachanja, hivyo inawashauri watumishi pia tutumie fursa hii kuchanja na kuacha kusikiliza maneno ya watu wasiyokuwa na weledi wa masuala ya afya,” alisema Prof. Msanjila.

Habari Kubwa