Gomes atangaza mechi nne za kuishusha Yanga

14Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Gomes atangaza mechi nne za kuishusha Yanga
  • ***Kuanza na Mtibwa leo kwa Mkapa, awachambua pia Waarabu wa Algeria na Kaizer Chiefs CAF, asema...

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema ana uhakika watazitumia vema mechi nne zilizopo mbele yao kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa malengo yao makubwa ni kutetea ubingwa huo.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes

Simba ambayo itashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa leo saa 1:00 usiku kuikaribisha Mtibwa Sugar, imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa kileleni mwa msimamo wa Kundi A, lililokuwa likimjumuisha bingwa mtetezi, Al Ahly ya Misri iliyomaliza nafasi ya pili, AS Vita ya DR Congo na Al-Merrikh ya Sudan iliyoburuza mkia.

Baada ya mechi ya leo, Simba itashuka katika Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga Jumapili kuivaa Mwadui FC, kisha  siku tatu baadaye itapambana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoka kabla ya Aprili 24, mwaka huu kutua jijini Mwanza kuvaana na Gwambina FC.

Hadi sasa Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 46 baada ya mechi 20, huku Yanga ikiwa kileleni na alama zake 51 zilizotokana na michezo 24 wakati Azam FC iliyoshuka dimbani mara 25, ikiwa na pointi 47 katika nafasi ya pili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na mwandishi wetu juzi, Gomes alisema baada ya mechi nne zijazo kuanzia ya leo dhidi ya Mtibwa Sugar watakuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

"Yaliyopita yamepita tumefuzu robo fainali ambayo tutacheza mwezi ujao, kwa hiyo tuna muda wa kujiandaa, sasa tunataka kuelekeza nguvu kwenye ligi kwa sababu ligi ni lengo letu kuu, lazima tuchukue nafasi ya kwanza haraka, tunataka kucheza Ligi ya Mabingwa kila mwaka.

"Natarajia utashi na hamasa kubwa kwa wachezaji wangu na ninahakika nitacheza na wachezaji wangu bora," alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.

Kuhusu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Gomes alisema: "Kwa ukweli tuna furaha kufika robo fainali kwani kundi letu lilikuwa gumu sana, tulianza kwa kucheza mechi ngumu na kiufundi mkubwa dhidi ya AS Vita, na kisha tukampiga Al Ahly hapa nyumbani, ninauhakika kwa sasa Simba ni moja kati timu bora Afrika, hivyo kwa sasa hatumhofii yeyote.

"Tunaziheshimu timu zote, tupo huru kucheza na timu yoyote, CR Belouizdad na MC Alger nazijua vizuri maana nilifundisha soka Algeria pia Kaizer Chiefs naifahamu, hatutakiwi kuchagua, Mungu atatupa timu moja baada ya hapo tutatakiwa kucheza kwa kujiamini na heshima. Katika mashindano ya CAF tunaweza kuvuka robo fainali kama tutakuwa na nidhamu na kucheza kwa nidhamu kama ambavyo tunacheza wakati wote," Gomes alisema.

Kocha huyo alisema hajutii  kuondoka Al-Merrikh Januari na kujiunga na Simba na amekuwa akishangazwa na hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo hususan katika mechi dhidi ya Al Ahly wakishinda bao 1-0.

 "Ni ajabu, uwanja ulijaa mashabiki na kiukweli walitupa nguvu, kama unataka kwenda mbali kwenye mashindano ya Afrika na Ligi ya Mabingwa, unahitaji mashabiki wenye hamasa, tuna kazi ya kufanya na Simba, na nina hakika tukiwa pamoja katika televisheni na uwanjani, tunaweza kutengeneza njia nzuri katika mashindano haya.

Lakini kuelekea mechi ya kesho, kwa upande wa Kocha wa Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas, yeye alisema Simba ni miongoni mwa timu bora Afrika kwa sasa ambayo inacheza vizuri kwa pamoja, lakini wamejipanga kuona ni namna gani watawakabili.

"Utakuwa ni mchezo mzuri wa kufunguka zaidi kwa sababu timu zote zinacheza, kama unajua Mtibwa ni timu ya kucheza na Simba na wenyewe ni timu ya kucheza," alisema.

Habari Kubwa