IGP Sirro aagiza uchunguzi kwa polisi aliyemwambia Mbowe hashindi

11Oct 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
IGP Sirro aagiza uchunguzi kwa polisi aliyemwambia Mbowe hashindi

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amesema timu kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo iko mkoani Kilimanjaro kufanya uchunguzi wa video ya ofisa wa polisi anayedaiwa kumwambia Mgombea Ubunge wa Hai (CHADEMA), Freeman Mbowe, hatashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Video hiyo iliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii katikati ya wiki hii, inamwonyesha ofisa huyo wa polisi akijibizana na Mbowe, ofisa huyo akisikika akisema 'utamshinda yule? huwezi kumshinda, unawadanganya wananchi kuwa utamshinda."

Katika majibizano hayo, ofisa huyo aliyekuwa na mavazi ya Jeshi la Polisi, pia alisikika akimwambia Mbowe kuwa anasababisha watu wanamfuata na kumtaka aingie kwenye gari.

“Mnafanya watu wanakuja, ingia kwenye gari tuondoke," alisikika ofisa huyo huku Mbowe akimjibu "sawa, msifukuzie watu wangu, watu wanifuate niwakimbie, hapana!”

Baada ya Mbowe kutoa kauli hiyo, ofisa huyo akasema: “Huwezi kumshinda hata ufanyeje, humshindi, ingia kwenye gari uondoke, yaani mawazo yako unawadanganya wananchi utamshinda, humshindi."

Akizungumza kuhusu video hiyo jana, IGP Sirro alikiri kuiona na kuweka wazi kwamba, tayari timu kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi imekwenda kulichunguza tukio hilo kwa kuwa kabla ya kufanya uchunguzi, hawapaswi kulaumu pande zote mbili.

“Nimeiona video hii na tunavyozungumza, timu yetu kutoka Makao Makuu tayari imekwenda kuchunguza hilo tukio kuona kuna nini. Suala la majibu kwamba utashinda au utashindwa, hiyo siyo kazi ya polisi, ni kazi ya tume (Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC).

"Tunachunguza, tukiona kuna jambo la ukweli kutokana na ile video tuliyoiona, basi tutachukua hatua dhidi ya huyo ofisa. Jeshi lina kanuni zake na tuna kanuni za kudumu, wanasema 'Police General Order', ile inatuongoza sana, lakini pia tuna sheria za Jeshi la Polisi na za maofisa wasaidizi pia na maelekezo.

“Kimsingi kamanda anapokwenda tofauti, polisi ofisa anapokwenda tofauti, ipo miongozo na maelekezo yanayotawala utendaji wetu, basi tunamwajibisha kwa mujibu wa taratibu zetu, kwa hiyo wanaelewa," alisisitiza.

 

Habari Kubwa