Ijue siri mishahara watumishi wa umma kutopandishwa miaka sita

29May 2021
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Ijue siri mishahara watumishi wa umma kutopandishwa miaka sita
  • *Bunge, wanasheria waipa mbinu serikali kuepuka athari hasi kiutendaji

KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, ulitolewa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu za kiuchumi na kisheria zilizochangia uamuzi wa serikali wa kutopandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa miaka sita mfululizo.

Vilevile, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, akaweka bayana kwamba tatizo hilo ni la kihistoria, akibainisha lilianza mwaka 1980 wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Endelea na sehemu ya pili kujua undani wa mustakabali wake.

---

Ili kutimiza ndoto za watumishi wa umma za kuongezwa kwa ujira wao, Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (CHADEMA), anaishauri serikali kuruhusu taasisi za nje ya nchi kuja kufanya tathmini ya kifedha (credit rating).

 

Mdee ambaye katika Bunge la 11 alikuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, anasisitiza kuwa kwa kuruhusu taasisi huru kufanya tathmini ya kifedha nchini, kutaisadia Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu badala ya mikopo ya kibiashara yenye masharti magumu inayopewa sasa.

Anasema uamuzi huo utaleta ahueni kwenye Deni la Taifa ambalo ni sehemu ya mzizi mkuu wa kutopandishwa kwa mishahara ya watumishi wa umma.

"Kwa hali ilivyo sasa, ninaona kuna haja kuruhusu taasisi huru zije kutufanyia 'credit rating' ili kutusaidia kama taifa kujua deni letu halisi likoje.

"Kwa kutofanyiwa 'credit rating', benki nyingi za kimataifa zenye mikopo ya riba nafuu zitaendelea kutuogopa kutukopesha kwa sababu hazina uhakika kama tutalipa au la. Matokeo yake tutaendelea kukopa kwa masharti magumu ya kibiashara," Mdee anashauri.

Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, pia ana ushauri kwa serikali kufanya marekebisho katika Sheria ya Deni la Taifa ambayo ina miaka zaidi ya 40 tangu kutungwa kwake.

Anapendekeza marekebisho ya sheria yalenge kukabiliana na kupaa kwa Deni la Taifa kwa kuitaka serikali kuwa makini katika ukopaji mpya, akisisitiza inapaswa kukopa kutekeleza miradi ambayo ina uhakika itarejesha fedha.

"Sheria yenyewe ya Deni la Taifa imepitwa na wakati. Ni sheria ya miaka ya 1970. Hoja hapa ni kwamba tuwe na sheria inayoitaka serikali kukopa pale tu inapohitaji kutekeleza miradi yenye uhakika wa kurejesha fedha na kulipa deni," Mdee anasema.

HALI YA DENI LA TAIFA

Februari 8 mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Sillo Baran, aliliarifu Bunge kuwa hadi Desemba mwaka jana, Deni la Taifa lilikuwa limefikia Sh. trilioni 59 kutoka Sh. trilioni 54.8 Desemba 2019, sawa na ongezeko la asilimia 7.6.

Baran alifafanua kuwa deni la ndani ni Sh. trilioni 16.2 na deni la nje ni Sh. 42.8 na kwamba ongezeko hilo limesababishwa na mikopo mipya ambayo serikali imeichukua ili kugharamia miradi ya maendeleo.

"Kamati inaishauri serikali kukamilisha haraka mchakato wa nchi yetu kufanyiwa 'credit rating' ili kuiwezesha serikali kupata mikopo nafuu na kwa urahisi," Baran alisema.

Nipashe inatua mezani kwa Dk. Mwajuma Kadilu, Mkuu wa Idara ya Sheria za Madai na Jinai katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambaye anaishauri serikali kupandisha mishahara ya watumishi wa umma ili kukidhi matakwa ya kisheria.

Dk. Mwajuma ana ufafanuzi zaidi katika hili akisema: "Sheria za kazi tunazozitumia sasa zilitungwa mwaka 2004 na zinataka kila baada ya miaka mitatu mabadiliko ya ujira, kukielekezwa viwango tofauti vya mishahara kulingana na sekta na skimu za utumishi.

"Mwaka 2007 tukawa na mabadiliko katika ujira wa watumishi, mwaka 2010 tukawa na mabadiliko na mengine yalishuhudiwa mwaka 2013 ambayo ndiyo 'wage order' inayotumika hadi sasa.

"Kwa maoni yangu, hii imepitwa na wakati. Kwa mfano, inasema kima cha chini cha mshahara wa 'house girl' (msichana wa kazi za nyumbani) unayeishi naye na anayekutegemea kwa chakula, malazi, matibabu na mengineyo, uwe Sh. 40,000 na kama anakuja na kuondoka umlipe Sh. 60,000.

"Kwa gharama halisi za maisha, viwango hivyo ni vidogo mno. Kwanini hatukuwa na viwango vipya vya mishahara mwaka 2017 na 2020 kama sheria inavyotaka?

"Je, ni Labour, Social and Economic Council haikutimiza wajibu wake au bodi za mishahara? Ni mawaziri wa kazi na yule wa utumishi wa umma wametukwamisha? Kuna sababu nyingine tofauti na hii ya hali ya uchumi wa nchi?" Dk. Mwajuma anahoji.

Kwa mujibu wa TUCTA, tangu mwaka 2014, watumishi wa umma nchini hawajashuhudia ongezeko katika ujira wao wa kila mwezi.

Habari Kubwa