JPM aagiza msako madaktari waliozikimbia ajira serikalini

31Jan 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
JPM aagiza msako madaktari waliozikimbia ajira serikalini

RAIS John Magufuli ameagiza madaktari waliohama Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tabora na kukimbilia hospitali binafsi kwa kigezo cha maslahi, wafuatiliwe waliko na hatua zichukuliwe dhidi yao.

Alitoa maagizo hayo jana wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura la Hospitali ya Rufani Mkoa wa Tabora, utakaogharimu Sh. milioni 616.3.

Rais Magufuli alihoji sababu za madaktari hao walioomba kuajiriwa serikalini na kuziba nafasi za wengine.

"Kwa sababu kazi ya udaktari ni kazi ya kumtolea Mungu sadaka, hata wauguzi hakuna anayeridhika na mshahara, kumbe huyo alipofika hapa akaondoka pamoja na mshahara wetu, kwanini asishtakiwe kwa wizi?" alihoji.

Kiongozi huyo wa nchi alipewa taarifa kuwa hospitali hiyo ina madaktari bingwa watano na walioondoka mpaka sasa ni watatu.

“Walisomeshwa na serikali? Warudishe hizo fedha, watafutwe ili kujua fedha zetu zipo wapi? Kwa sababu hakuna anayeridhika na mshahara, hata mimi siridhiki nao, hata manesi hawaridhiki lakini wanajituma.

“Tunataka wote matatizo yetu tuyatatue kwa pamoja, hatuwezi kuyatatua kwa siku moja, tunafahamu tunachukua hatua nyingi kuimarisha huduma za afya.

"Kulikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya, tumeajiri zaidi ya watumishi wa afya 14,000 katika kipindi cha miaka mitano," alibainisha.

Rais Magufuli alisema mwaka jana, waliajiri watumishi wa afya 1,000 na wamejenga hospitali za wilaya 102, hospitali za rufani tatu na vituo vya afya 487.

"Tulianza na hizo na baadaye tunaingia kwenye maslahi ya watumishi wa afya, tunajua wanafanya kazi kubwa ya kujitolea, ninawapongeza sana, mbona wewe hujakimbia? Kinachohitajika ni uzalendo.

"Wanawake wanaumwa, wengine wanatakiwa kufanyiwa upasuaji, wewe unakimbia, mfuatilie huyo daktari aliyekimbia hapa na uifuatilie na hiyo hospitali ikiwezekana tunamfungia daktari na kuifungia hospitali aliyokwenda huko, ili watu wajifunze kwamba Wizara ya Afya siyo ya kuchezewa tu.

"Mtu anasomeshwa kwa fedha za watu maskini na wanapata mkopo kwa asilimia 100, halafu wanamaliza wanakimbia maslahi madogo.

"Si ungekimbia wakati unasoma. Fedha yetu umekula halafu unasema maslahi madogo, tunataka maslahi yaboreshwe, ila lazima tuanze na kimoja, huwezi kuboresha maslahi wakati hata hospitali huna, vifaa huna," alisema.

Rais Magufuli alisema suala la maslahi ya watumishi wanaliangalia kikamilifu kulingana na bajeti inavyokwenda.

"Wahudumu wa afya uzalendo unatakiwa kuwa mbele, nimesikia changamoto ya jengo hapa, nitazungumza na Waziri na TAMISEMI tuone namna ya kusaidia," alisema.

Rais Magufuli alisema ameambiwa kwa sasa hospitali hiyo ina chumba kimoja cha kuhudumia wagonjwa wa dharura ilhali kila siku wanapokea wastani wa wagonjwa 15 wa kundi hilo.

"Jengo hili lenye uwezo wa kupokea wagonjwa wa dharura 50 litaokoa maisha ya wananchi wa Tabora, mradi huu umefadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Afya (Global Fund), tunawashukuru kwa ufadhili huu," alisifu.

Akizindua miradi ya maji iliyotekelezwa mkoani humo, Rais Magufuli alisema hadi sasa vipo vituo 728.

"Kwa kazi hii ninawapongeza makandarasi na wahandisi na kabla sijasahau waziri alitoa ombi la mhandisi ambaye muda wa kustaafu umefika na kuomba aongezwe muda. Kwa kazi hii mliyofanya, ninamwongezea miaka miwili," alisema.

Rais Magufuli alisema fedha za utekelezaji mradi huo ni za mkopo kutoka Benki ya Exim ya India na kwamba ulianza Agosti 2017 na kukamilika Februari mwaka jana na sasa wako katika kipindi cha uangalizi kitakachokamilika mwezi ujao.

Alisema Serikali ya India ilitoa mkopo mwingine kwa Tanzania wa kutekeleza mradi wa maji Mlandizi, Kibamba, Lindi na Chalinze na kutoa Dola za Marekani  milioni 500 (sawa na Sh. trilioni 1.2) ili kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 28 pamoja na Zanzibar.

Alisema 2015 wakati wa kugombea Urais, wabunge wa Tabora walisema mkoa huo umesahaulika ndiyo maana aliagiza Sh. bilioni 617 zipelekwe ili kutekeleza miradi ya maji.

"Ninakuagiza Waziri wa Maji, hakikisheni wananchi wanapata maji, siyo maji yanabaki kwenye matenki, nimeagiza!

"Pia, ninataka maji haya yaliyofika Tabora, yafike Urambo, Sikonge na Kaliua, bahati nzuri zipo Sh. bilioni 25 zilizookolewa, zikatumike kutekeleza miradi kwenye hizo wilaya tatu," aliagiza.

Aliipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji huo na kuwaeleza kuwa awali, miradi mingi ilikuwa ikisuasua na sasa wameanza na mwelekeo wa kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.

Rais Magufuli alisema tatizo kubwa la Mkoa wa Tabora analoliona ni majungu mengi, akionya kuwa hayajengi na kuwataka viongozi waliopewa madaraka, wajenge umoja.

"Mwenyekiti wa maadili ya wabunge ni huyu hapa, lakini Tabora anapigwa vita, hamuwezi mkawa wabunge wote, uchaguzi umekwisha na mbunge ni Mwakasaka, umtake usimtake, Mwakasaka ataendelea kusaka miaka mitano.

"Kikubwa ni yale majungu majungu, mlinichagua niseme ukweli wa Mungu ndiyo maana ninasema hapa mbele yenu, ninajua na mimi siyo ajabu nikitoka hapa nitapigwa majungu, mpige litavunjika huko, ninaendelea kwenda mbele," alisema.

Habari Kubwa