JPM aahidi kupandisha mishahara

06Sep 2020
Gwamaka Alipipi
Mara
Nipashe Jumapili
JPM aahidi kupandisha mishahara

MGOMBEA urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameahidi kupandisha mishahara ya watumishi wa umma ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atashinda tena kuongoza nafasi hiyo.

Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, akisalimiana na Mgombea
Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Dk. John Pombe Magufuli, wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu katika uwanja wa Mkendo, mjini Musoma, Mkoa wa Mara jana. PICHA: IKULU

Amesema hakutekeleza ahadi hiyo katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake kwa kuwa alitaka kukamilisha kwanza baadhi ya mambo muhimu ya kitaifa ikiwamo ujenzi wa hospitali, zahanati, huduma ya elimu na miradi mingine ya maendeleo.

Alitoa ahadi hiyo jana wilayani Musoma mkoani Mara wakati akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM waliojitokeza katika Uwanja wa Mukendo kumsikiliza.

“Ninawaahidi wafanyakazi, kabla sijaondoka madarakani nitahakikisha nimeongeza mishahara yenu… sikutaka kuongeza awali kwa sababu kuna baadhi ya vitu ilibidi tukamilishe kwanza ndipo lifuate," alisema.

Dk. Magufuli alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya watumishi walioajiriwa ni 61,000, na serikali yake imelipa maslahi yao, pensheni na malimbikizo zaidi ya Sh. bilioni 200.

"Mtu anakuja anasema hatupandishi mishahara ya wafanyakazi, hivi ukimpandisha mtu daraja, mshahara wake unabaki palepale?

"Masuala ya kuongeza mshahara halafu unapandisha nauli, bidhaa, hapana! Tuliamua kwanza kutoa elimu bure na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Sh. bilioni 450 (kwa mwaka).

Tungeweza kuwadanganya wafanyakazi tumepandisha mshahara, tuliamua kuanza kusomesha watoto wa maskini bure.

"Ndiyo maana katika hii llani ya CCM inazungumzia maslahi ya wafanyakazi, wakulima, wavuvi na kwa wafanyabiashara. Ilani hii inawapenda sana, tumewajali wafanyabiashara wadogo, miaka ya nyuma ukisimama mgambo anakuja kukusumbua," alisema.

Dk. Magufuli pia aliwaahidi Watanzania kuwa atatekeleza mambo aliyoyapanga Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ndani ya miaka mitano kwa kasi kubwa.

Vilevile, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utawala wake, atahakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.

”Hata suala la bima Tanzania tuko mbele sana, katika mipango ya baadaye tunataka kutoa bima kwa watu wote.

Ukurasa wa 136 wa Ilani ya CCM inazungumzia kuimarisha mfumo wa afya nchini ikiwamo huduma ya CHF na NHIF. Mtakapotuchagua, tunataka kuipanua kwa Watanzania wote na wakati huo tutakuwa na Watanzania milioni 60,” alisema.

Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, amejenga hospitali za wilaya za Bunda, Butiama, Musoma, Musoma, Rorya, Serengeti na Tarime pamoja na vituo vya afya vinane na zahanati 27 kwa Sh. bilioni 25.1.

Alisema serikali yake pia imejenga shule za sekondari 35 na za msingi 102, ujenzi wa nyumba 152 za walimu, ukarabati wa vyuo vya walimu na kutoa Sh. bilioni 49.95 mkoani Mara.

Kwenye sekta ya maji, Dk. Magufuli alisema miradi 38 imetekelezwa kwa Sh. bilioni 68.4. Kati yake, miradi 17 imekamilika huku mingine ikiwa katika utekelezaji.

Mgombea huyo wa CCM pia alisema vijiji 411 mkoani Mara vimefikiwa na huduma ya umeme kati ya 458 kwa gharama ya Sh. bilioni 105.4.

Habari Kubwa