JPM atangaza maelfu ajira za walimu

20Jan 2021
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
JPM atangaza maelfu ajira za walimu

RAIS John Magufuli, amesema serikali inatarajia kuajiri walimu wapya 5,000 ili kuimarisha sekta ya elimu na kupunguza tatizo la ajira nchini.

Rais John Magufuli

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukoba mkoani Kagera jana baada ya utiaji saini kati ya Tanzania na Kampuni ya Madini ya LZ Nickel, Rais Magufuli alisema serikali imejizatiti katika kukuza sekta ya elimu nchini.

Alisema kuwa tangu aingie madarakani, wameshaajiri zaidi ya walimu 30,000 na hivi karibuni walitangaza nafasi za ajira 8,000 na sasa wanatangaza nafasi za walimu 5,000 na kati yao, watakwenda Bukoba.

Alisema wanataka suala la elimu lizingatiwe nchini, akisisitiza kuwa taifa lolote linalothamini elimu, ndiyo linalothamini maendeleo ya kweli na ndiyo sababu waliamua kuweka mkakati wa elimu bure.

"Katika kipindi cha miaka mitano, kumetumika kiasi cha Sh. trilioni 1.1 kushuhulikia suala la elimu na tutaendelea kufanya hivyo na katika elimu ya juu tumetumia zaidi ya Sh. bilioni 450 kwa kila bajeti katika kila mwaka," alisema.

Rais Magufuli pia alionya kuhusu utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi, akidokeza kuwa angetamani viboko viendelee shuleni.

“Ninajua hilo hamtalipenda, lakini hiyo ndiyo njia pekee ya kumsaidia mtoto, lakini ninajua watoto wangu ni wapole na wanafuata masharti yote, hao viboko havitawahusu,” alisema.

Awali, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Madini kuweka utaratibu utakaowezesha mradi wa uchimbaji wa madini ya Nickel katika eneo la Kabanga wilayani Ngara, kuanza haraka baada ya Serikali ya Tanzania kutia saini makubaliano ya awali na Kampuni ya LZ-Nickel.

Rais alisema mradi wa Kabanga Nickel ulianza tangu mwaka 1976 na sasa ni muda mwafaka madini hayo kuanza kuchimbwa, ili wananchi wa Ngara wanufaike.

"Kwa bahati mbaya, kipindi hicho chote hakupatikana mwekezaji wa kuchimba madini ya Kabanga Nickel kwa manufaa ya wananchi wa Ngara, mkoa mzima na taifa kwa ujumla," alisema.

Alisema ili kutekeleza mradi huo kwa usahihi, Kampuni ya LZ-Nickel kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, wametengeneza kampuni tanzu iitwayo Tembo Nickel.

"Ninafahamu katika nia njema ya serikali watatokea wapingaji maana kuna waliokuwa wanautaka na hao wapingaji watashirikiana na Watanzania wa hapahapa, lakini biashara ya wivu ndiyo inatawala hapa duniani.

"Tumedanganywa muda mrefu eti wanabeba mchanga kumbe tunaibiwa, na kama ni kuibiwa tumeibiwa sasa, hatuwezi kukubali kuendelea kuibiwa, na wananchi wa Ngara wamekaa kwenye mali, lakini ni maskini," alisema.

Rais Magufuli pia aliagiza Wizara ya Ujenzi kutangaza tenda haraka kutengeneza barabara ya Nyakahura hadi Rusumo wilayani Ngara ambayo inaunganisha Tanzania na Rwanda.

Alisema sekta ya madini inaendelea kukua, akibainisha kuwa wakati anaingia madarakani, Tanzania ilikuwa inapata Sh. bilioni 168, lakini sasa imeongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 528 kwa mwaka.

Wawekezaji wa mradi huo wametoka katika nchi za Marekani, Australia na Uingereza.

*Imeandikwa na Lilian Lugakingira (KAGERA) na Maulid Mmbaga (DAR)

Habari Kubwa