JPM azindua daraja la Kijazi Ubungo

24Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
JPM azindua daraja la Kijazi Ubungo

Rais John Magufuli, amefanya uzinduzi wa daraja la juu la Ubungo lililopewa jina la aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (Kijazi Interchange) aliyefariki dunia Februari 17, 2021.

Rais Magufuli amezindua barabara hiyo leo Jumatano Februari 24, 2020 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu jijini Dar es Salaam.

Amewasili eneo hilo saa 3:50 asubuhi na kufanya uzinduzi kwa kukata utepe na baadaye alikwenda kuvuta kamba na baada ya kumaliza alishuka eneo la chini la daraja hilo na kuzindua rasmi kwa kufunua jiwe la msingi lililowekwa eneo hilo.

Akizungumza na wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema kuwa daraja hilo litarahihisisha usafiri ndani ya jiji hilo pamoja na uchumi kuzidi kukua kwa kasi.

"Ninafahamu kulikuwa na foleni hapa iliyosababisha watu kuchelewa kufanya kazi zao kwa uhakika kutokana na kuchelewa kufika kwenye kazi zao sasa hilo limekwisha ndugu zangu wana Dar es Salaam. Leo nawaambia ukweli kuwa ni siku ya furaha ndani ya mkoa wetu maana tuna hii interchange ya KIjazi sasa itapunguza foleni," amesema Magufuli.

Kabla ya kukata utepe mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale amesema Kijazi interchange lina urefu wa mita 700 barabara ya kutoka Buguruni kwenda Mwenge na umbali wa mita 260 kutoka Kimara kwenda Manzese na kwamba barabara za chini zina umbali wa kilomita tano.

Habari Kubwa