Kachero adai alivyotaka kuhongwa na mshtakiwa kesi dawa za kulevya

16Feb 2021
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Kachero adai alivyotaka kuhongwa na mshtakiwa kesi dawa za kulevya

SHAHIDI wa tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya ulimaji wa dawa za kulevya aina ya bangi na kufanya mauzo ndani na nje ya nchi, inayomkabili mwekezaji wa kigeni, amedai kuwa mshtakiwa huyo alimwomba wamalizane kimyakimya kwa dau la Sh. milioni 10.

Kesi hiyo inamkabili raia huyo wa kigeni, Damian Jankowski na wenzake watatu, na kuwa mshtakiwa huyo alimwahidi shahidi huku akiahidi kumlipa pesa kila mwezi.

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2020, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Bernazitha Maziku, inawakabili Jankowski raia wa Poland na wastakiwa wenzake Eliwaza Pyuza, Hanif Kanani na Boniface Kessy.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake jana mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Verdiana Mlenza, Mkaguzi wa Polisi, Inspekta Hassan Msangi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), alidai wakati anafanya upekuzi nyumbani kwa Jankowski, mfanyabiashara huyo alimuita pembeni na kumweleza kwamba yuko tayari kumlipa Sh. milioni tano ili aachane naye.

Baada ya kuona ofisa huyo wa polisi hayuko tayari, alipanda dau na kumwambia atampa Sh. milioni 10 na vilevile kila mwisho wa mwezi awe anaenda kwake kuchukua pesa, lakini alikataa na kumwambia binafsi yuko kazini na hawezi kuhitaji hivyo vitu, anaendelea na kazi yake.

Katika hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni kulima dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 11 (1) (a) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015.

Mshtakiwa wa kwanza, pili na wa tatu wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 8 mwaka jana, huko katika eneo la Njia Panda ya Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, walikutwa wamelima miche ya bangi 729.

Wakati kosa la pili ambalo linawakabili mshtakiwa wa kwanza, pili na wa tatu, ni kusafirisha bangi kinyume na kifungu cha 15A (1) (2) (C) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 15 ya Mwaka 2017 kama ilivyofanyiwa marejeo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao pia wanadaiwa kukutwa na kilogramu 15.6 za bangi katika eneo la Shirimatunda, Manispaa ya Moshi, Februari 8, mwaka jana.

Kosa la tatu ni kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 15A (1) (2) (C) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marejeo kifungu cha 9 cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 15 ya Mwaka 2017.

Na kosa la nne ni matumizi ya dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 18 (a) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015.

Mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo ni pamoja na Mkemia, Joyce Labani na Erasto Lawrence kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na John Msirikali ambaye ni mtunza vielelezo kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka akisaidiana na Verdiana Mlenza, wakati mshtakiwa wa kwanza, wa pili na watatu katika kesi hiyo, wanatetewa na Wakili FayGrace Sadala. Kesi hiyo itaendelea tena leo.

Habari Kubwa