Kada CHADEMA adaiwa kufanyiwa unyama na wasiojulikana

09Oct 2020
Allan Isack
Arusha
Nipashe
Kada CHADEMA adaiwa kufanyiwa unyama na wasiojulikana

KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Evarist Rite, mkazi wa Narumu, Hai mkoani Kilimanjaro, ameokotwa akiwa amejeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana.

Mtu huyo aliokotwa jana akiwa ametelekezwa kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, mji mdogo wa Kikatiti, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Elias Mungure, alisema majira ya saa 11:00 jioni ya juzi, alipigiwa simu na wananchi na baadhi ya makada wa chama hicho wakimweleza kuwa kuna kada wa chama wamemkuta ametupwa barabarani.

“Tuliondoka vijana wetu kwenda eneo la tukio na tulipofika, tulimkuta Evarest akiwa ametupwa barabarani, anavuja damu kwenye ulimi, mikono, vidole, sehemu za siri na amevunjwa meno mawili ya mbele,” alisema Mungure.

Kwa mujibu wa Mungure, mtu huyo alitupwa karibu na kituo cha mafuta na kwamba waliofichua taarifa hizo ni pamoja na wafanyakazi wa kituo hicho, ambao walipiga simu Kituo cha Polisi na askari kufika eneo la tukio na kumhoji kada huyo.

“Kutoka kituo cha mafuta hadi kituo cha polisi kuna umbali wa mita 100 na baada ya hapo tulisafiri hadi Wilaya ya Hai, tulichukua PF3 (fomu ya polisi namba tatu) kwa ajili ya matibabu. “Baada ya kuchukua fomu hiyo, tulimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Tuliwasiliana na viongozi wetu wa chama Wilaya ya Hai. “Walipofika hospitalini hapo, walithibitisha kumfahamu kada huyo na walisema kuwa walikuwa wamempangia majukumu ya kwenda kuchukua mabango ya chama,” alisema.

Mungure alisema walipofika eneo la tukio walimkuta kada huyo akiwa anatokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi (ACP) Salum Hamduni, alisema bado hajapokea taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo.

Habari Kubwa