'Kimbunga cha Samia' chatikisa TANESCO

26Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
'Kimbunga cha Samia' chatikisa TANESCO

RAIS Samia Suluhu Hassan amerejea nchini akitokea Marekani na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, akiwaondoa 'vigogo' wa Shirika la Umeme (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam jana mchana, Rais Samia alilakiwa na wananchi waliobeba mabango yenye ujumbe wa kumpongeza kwa aliyoyafanya akiwa Marekani alikokwenda kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Muda mfupi baada ya kuwasili nchini, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikibainisha kuwa Rais Samia amemteua Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO. Kabla ya uteuzi huo, Issa alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi (PDB)

Taarifa hiyo ya Ikulu ilibainisha kuwa Rais Samia amemteua Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO. Kabla ya uteuzi huo, Chande alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika na anachukua nafasi ya Dk. Tito Mwinuka.

Rais Samia pia amemteua Michael Minja kuwa Kamishna wa Petrol na Gesi, Wizara ya Nishati. Kabla ya uteuzi huo, Minja alikuwa Mkurugenzi Mkuu – TIPPER.

Taarifa hiyo ya Ikulu pia ilibainisha Mkuu wa Nchi amemteua Felschemi Mramba kuwa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu. Kabla ya uteuzi huo, Mramba alikuwa Mshauri Mkuu wa Kiufundi  – TANESCO Training School.

Pia amemteua Hassan Said kuwa Mkurugenzi Mkuu wa REA. Kabla ya uteuzi huo, Seif alikuwa Meneja wa Kanda Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki TANESCO. Said anachukua nafasi ya Amos Maganga.

Taarifa hiyo ya Ikulu ilibainisha kuwa uteuzi huo ulianza Septemba 23, mwaka huu, lakini haikubainisha sababu za kufanyika kwa mabadiliko hayo ya uongozi.

Katika taarifa hiyo, pia ilibainishwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, amewahamisha watumishi waandamizi watano toka TANESCO kwenda Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine.

Watumishi hao ni: Khalid James – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji; Raymond Seya – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Masoko; Isaac Chanje – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji; Nyelu Mwamaja – Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi; na Amos Ndegi – Mwanasheria wa TANESCO.

Mabadiliko hayo ya kiuongozi ndani ya mamlaka hizo mbili zinazoshughulikia nishati ya umeme nchini yamefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Rais Samia kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, akimteua Mbunge wa Bumbuli, January Makamba kushika wadhifa huo.