Maelekezo ada shule binafsi

27Jun 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Maelekezo ada shule binafsi

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa maelekezo ya ulipaji ada kwa shule binafsi na kuziagiza Kamati na Bodi za shule kufanya uchambuzi wa gharama inayopaswa kupungua kwa siku ambazo wanafunzi hawakuwa shuleni kutokana na janga la corona.

Pia, Wizara imeagiza wanafunzi wote kupokelewe na kuendelea na masomo bila kikwazo chochote ili kukamilisha muhula.

Maelekezo hayo yalitolewa jana na wizara hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa wizara hiyo, Sylvia Lupembe, kwa vyombo vya habari.

Katika taarifa hiyo, Lupembe alisema kamati na bodi hizo zinatakiwa kufanya uchambuzi wa malipo ya chakula na usafiri na tathmini hiyo izingatie ratiba mpya ya mihula iliyotolewa na wizara.

“Kulingana na Sheria ya Elimu sura namba 353 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, uendeshaji wa shule unasimamiwa na kamati au bodi za shule, vyombo ambavyo vimeundwa kwa mujibu wa sheria hiyo,”alisema.

Aliwataka wamiliki wa shule kuzingatia sheria hiyo na kuzipa nafasi bodi kutekeleza majukumu yake kulingana na matakwa ya sheria.

Alisema wizara inaelekeza wanafunzi wote wapokelewe kwa ajili ya kuendelea na masomo ifikapo Juni 29, mwaka huu na kusisitiza kusiwapo na nyongeza yoyote ya ada.

“Kulingana na ratiba iliyotolewa na wizara, wanafunzi wanatarajia kukamilisha masomo kama inavyoelekezwa na mihtasari ya madarasa waliyopo, hivyo ada za shule zilipwe kulingana na makubaliano yaliyoafikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo,” alisema.

Kadhalika, wazazi wanatakiwa kuzingatia kiwango cha ada kukadiriwa kwa kuzingatia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule, ambazo ziliendelea kuwapo hata muda ambao shule zilikuwa zimefungwa.

“Gharama hizi ni pamoja na mishahara ya watumishi, ankara za umeme na maji,” alisema.

Habari Kubwa