Magufuli afuta kikokotoo kipya

29Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli afuta kikokotoo kipya

YAMETIMIA. Ndivyo ambavyo mtu anaweza kuelezea kutokana na hitimisho la Rais John Magufuli kwa kufuta kikokotoo cha mafao baada ya mfanyakazi kustaafu kilichokuwa kimependekezwa katika kanuni za Sheria ya Mifuko ya Jamii.

Rais John Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kulia), na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na viongozi wa wafanyakazi na wa mifuko ya hifadhi ya jamii wakiwa wameshikana mikono kwa furaha huku wakiimba wimbo wa hamasa wa mshikamano wa wafanyakazi wa "Solidarity Forever" baada ya kuwasikiliza hoja zao, kuwahutubia na hatimaye kulipatia jawabu swala la vikokotoo vya wafanyakazi alipokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Hatua hiyo ya Rais Magufuli ilifikiwa jana katika kikao cha pamoja kati yake na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wakiongozwa na viongozi wakuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), mifuko ya hifadhi ya jamii, waajiri na serikali kupitia wizara yenye dhamana ya hifadhi ya jamii.

Kikao hicho cha Rais na wadau hao wa hifadhi ya jamii, kiliitishwa mahsusi kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mvutano uliokuwapo baina ya vyama vya wafanyakazi na wadau kwa upande mmoja na SSRA kwa upande mwingine.

Lakini kubwa zaidi, ni kutokana na kilio kutoka kwa wafanyakazi kuwa kikokotoo cha 1/580 cha mafao mzigo na mateso kwa mstaafu ambaye amefanya kazi kwa heshima kwa zaidi ya takriban miaka 30.

Awali, wakati wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wadau, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, alisema kikokotoo cha mafao mapya ni kizuri kwa sababu kina manufaa kwa wastaafu tofauti na kile cha mwanzo.

Katika maelezo yake, Isaka alisema baadhi ya wastaafu walikuwa wakipokea mafao kidogo tofauti na kikokotoo kipya lakini sasa watanufaika kwa kuwa watapokea kiasi kikubwa cha mafao huku akitoa takwimu mbalimbali kujenga msingi wa hoja yake.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema: “Hayo mahesabu (hesabu) ni ‘too academic’ (ya kitaaluma zaidi) na yanachanganya watu.” Akihitimisha mjadala huo baada ya wadau wa pande zote kuzungumza kutokana na wanavyoona, Rais Magufuli alisema kikokotoo hicho kimeleta mkanganyiko na tahariki miongoni mwa wafanyakazi na hata wengine kukataa tamaa.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alisema kikokotoo hicho, hakitatumika tena na badala yake kanuni ya mafao itakayotumika ni ile ya zamani kabla ya kuunganishwa kwa mifuko kutoka sita na kuwa miwili.

“Formula (kikokotoo) hii imewa- ‘frustrate’ (imewavuruga na kuwachanganya) wafanyakazi. Kanuni zilizokuwa zikitumika kabla ya kuunganishwa kwa mifuko zitaendelea kutumika,” alisema.

Kwa mantiki hiyo, wastaafu kama vile walimu, ambao walikuwa wanachama wa uliokuwa Mfuko wa Pensheni wa PSPF wataendelea kupata asilimia 50 ya mafao kwa mkupuo na wale wa lililokuwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wataendelea kupata asilimia 25.

Hata hivyo, Rais alisema malipo hayo ya pensheni na mafao yatafanywa katika kipindi cha mpito kuanzia sasa hadi mwaka 2023 na kwamba hadi kufikia wakati huo, kanuni mpya ya mafao itakuwa imepatikana kupitia wadau wote wa hifadhi ya jamii kwa maana ya serikali, wafanyakazi na waajiri.

“Kwanza kustaafu ni heshima na siyo mateso. Mtu amefanya kazi kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka 30 na matokeo yake unampa masharti kuwa atapata mafao kidogo. Utampangiaje mtu kuwa sasa utachukua kiasi fulani halafu kingine tutakutunzia, huu ni wema gani?” Hii haiingii akilini hata kigogo kwa mtu yeyote,” alisema.

“Mwalimu aliyefundisha kwa uaminifu miaka 40 hadi chaki zimemharibia macho na aliowafundisha wamekuwa na mishahara mikubwa na wengine ndio wakurugenzi wa hifadhi ya jamii. Akitaka kuchukua mafao yake unamwambia nitakupa kidogo ili ukaishi, aliyekwambia nani ataishi? "Mawaziri, wabunge wanachukua hela yao yote, halafu uwaambie wengine utachukua kidogo kidogo kila ukija, hawatakubali. Kwenye reality (uhalisia), hata mimi hainingii akilini, " alisema Rais.

Aliongeza kuwa: “Unapofanya jambo lolote juu ya mwingine, fikiria ingekuwa kwako uingekuwaje? Kwa hiyo ni lazima tujali na wengine pia badala ya kufanya mambo ya kuwaumiza,” alisisitiza.

Rais alisema kabla ya muda huo wa mpito kumalizika, wadau wawe wamepata kanuni mpya ya mafao huku akisisitiza kuwa hata kama itakuwa asilimia 60 hata 70 badala ya 40 waliyoomba yuko tayari kukubali ili mradi hali ya ukwasi wa mifuko ya jamii iwe nzuri.

SHANGWE ZALIPUKA

Baada ya Rais Magufuli, ambaye muda mwingi alikuwa akishangiliwa na wafanyakazi kuhitimisha suala hilo, ukumbi ulilipuka shangwe huku wafanyakazi wakiimba nyimbo za mshikamano na wakiwa wawameshikana mikono pamoja na Rais. Pia wimbo “Tuna imani na Magufuli… Oya, Oya, Oya… Magufuli Kweli, Kweli, Magufuli Kweli Kweli Magufuli, Magufuli Kweli…” ulichukua nafasi hali iliyoonyesha kuwa wafanyakazi wana imani na Rais Magufuli baada ya kukata mzizi wa fitina wa sakata hilo.

MWANZO WA SAKATA

Januari, mwaka huu, Bunge lilipitisha sheria ya hifadhi ya jamii, ambayo pamoja na mambo mengine iliunganisha mifumo ya hifadhi ya jamii kutoka sita na kuwa miwili. Mifuko iliyokuwa awali ni Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Mfuko wa Pensheni wa PPF, Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) na NSSF.

Kutokana na kuunganishwa kwa mifuko hiyo, iliundwa mifuko miwili mipya ambayo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta Binafsi na Isiyo Rasmi (NSSF) na ule wa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF).

Hatimaye sheria hiyo ilitiwa saini na Rais kwa ajili ya kuanza kutumika lakini kabla ya kutumika rasmi, iliopaswa kutungiwa kanuni ambazo pamoja na mambo mengine, zingeainisha kikokotoo cha mafao.

Baada ya hapo, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) kwa kushirikiana na SSRA iliandaa semina kwa ajili ya wahariri wa vyombo vya habari mjini Dodoma kuelezea umuhimu wa kanuni hiyo, huku ikieleza kinagaubaga kwamba ni mkombozi kwa wafanyakazi.

Baadaye, SSRA ilitoa ufafanuzi juu ya kikokotoo hicho kipya kwamba mstaafu atapata mafao ya 1/580 kwa mkupuo kisha kuendelea kulipwa kila mwezi kwa muda wa miaka 12.5 na iwapo angefariki dunia kabla ya muda huo, mafao yake yatatumika kusomesha watoto wake.

UPINZANI UKAANZA

Baada ya SSRA kutoa ufafanuzi huo uliotokana na baadhi ya vyombo vya habari, hususani gazeti la Nipashe kuibua sakata hilo, ulianza upinzani kutoka kila upande huku Waziri Kivuli mwenye dhamana ya Kazi na Ajira, Ester Bulaya, akaibuka na kusema bunge lilidanganywa kuhusu jambo hilo.

Bulaya, ambaye ni Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), alisema wabunge walitaka kikokotoo hicho kiainishwe kwenye sheria lakini serikali ilisema itakiweka kwenye kanuni na matokeo yake ilitunga kitu alisema ambacho kinawakandamiza wastaafu.

Mbunge huyo ambaye awali alikuwa CCM kabla ya kujiunga na upinzani, alisema kutokana na kanuni hiyo kuwa kandamizi na mzigo kwa mfanyakazi, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni.

Wakati Bulaya akiweka bayana jambo hilo, wadau mbalimbali waliibuka na kulishambulia bunge kuwa limetunga sheria ambayo inawaumiza wananchi huku wakishangaa wabunge kutowajali wananchi wakati wao wanachukua mafao yao yote bila kukatwa chochote.

Jambo hilo lilimwibua Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye aliruka kimanga na kusema bunge linabebeshwa mzigo wa lawama lisiostahili kwa kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitungi kanuni bali sheria.

Ndugai alimsifu Bulaya kwa kuweka bayana jambo hilo huku akisisitiza kuwa kama kuna mtu yeyote anaona kanuni hiyo ni kandamizi anapaswa kuiwasilisha Bungeni kupitia Kamati ya Sheria Ndogo iliyo chini ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ili hatua zaidi zichukuliwe ikiwamo kuiagiza serikali kuifanyia marekebisho.

TUCTA YACHARUKA

Hatimaye Tucta iliibuka na kupinga kanuni hiyo kuwa itasababisha maumivu makali kwa wastaafu huku ikisisitiza kuwa miongoni mwao wanaweza kukumbwa na maradhi ikiwamo msongo wa mawazo na hata kupoteza maisha.

Tucta pia ilisema hata wakati wa majadiliano juu ya kanuni hiyo kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya serikali na waajiri kwa upande mmoja na Tucta upande mwingine, hatua iliyosababisha hata wakati wa upigaji kura upande wa serikali na waajiri ulishinda.

Kutokana na kanuni hiyo kuwa kandamizi, Tucta iliiomba serikali kurejea kwenye meza ya mazungumzo na wadau, wakiwamo wafanyakazi kupitia vyama vyao ili kuifanyia marekebisho kanuni hiyo.

Vyama takriban vyote vya wafanyakazi, vikiwamo Chama cha Walimu (CWT), Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu), Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (THTU), vilipinga kanuni hiyo huku vikisisitiza serikali kukaa meza moja na wadau ili kuleta mtangamano juu ya jambo hilo.

 

Habari Kubwa