Majaliwa mgeni rasmi maonesho ya madini

20Jul 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Majaliwa mgeni rasmi maonesho ya madini

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maonesho ya biashara na teknolojia ya madini Mkoani Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati akizungumza na vyombo vya habari juu ya maonesho ya Biashara na Teckolojia ya madini mkoani humo. PICHA MARCO MADUHU

Maonesho hayo yatafanyika kuanzia Julai 23 mwaka huu hadi Agost Mosi katika viwanja vya Butulwa, kata ya Oldshinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuwa maonesho hayo ni ya awamu ya pili, ambayo yamelenga kukuza sekta ya madini na biashara mkoani humo.

Amesema Mkoa wa Shinyanga una migodi mingi ya madini, hivyo kupitia maonesho hayo yatatoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza mkoani humo, pamoja na kuunganisha mtandao wa wafanyabiashara.

"Maonesho haya ya biashara na teknolojia ya madini mkoani Shinyanga, yatatusaidia kukuza uchumi wa Mkoa wetu, na pato la mtu mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla, na tuta yafungua Julai 23, na mgeni rasmi atakua waziri mkuu Kassim Majaliwa," amesema Dk. Sengati.

"Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye maonesho haya, kuja kuona madini live pamoja na wafanya biashara wajumuike ili wapate mtadao na kukuza biashara zao," ameongeza.

Mwenyekiti wa maonesho hayo, Kulwa Meshack, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani Shinyanga, amesema maonesho hayo ni fursa kwa wachimbaji na wafanyabiashara na watabadilisha uzoefu namna ya kufanya kazi zao.

Habari Kubwa