Masharti magumu usajili vijiji yaja

15Oct 2021
Munir Shemweta
Tabora
Nipashe
Masharti magumu usajili vijiji yaja

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, amesema kuanzia sasa hakuna kijiji kitakachosajiliwa bila kushirikisha wadau muhimu ili kuondokana na migogoro ya ardhi.

Hatua hiyo ni kutaka kuondoa mgongano uliojitokeza wakati wa kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 baada ya kubainika kuwa baadhi ya vijiji kusajiliwa ndani ya mipaka ya hifadhi.

‘’Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza TAMISEMI iwe inashirikisha wadau muhimu wakati wa kusajili vijiji ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi iliyojitokeza kwenye vijiji 975,’’ alisema Silinde juzi mjini hapa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, wakati Kamati ya Mawaziri nane ikishughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi, baadhi ya vijiji vimeonekana kuwa ndani ya hifadhi na wananchi wake wamekuwa wakishiriki uchaguzi ukiwamo ule wa serikali za mitaa.

Wadau muhimu watakaoshirikishwa katika usajili wa vijiji ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.

‘’Ofisi ya Rais TAMISEMI ndiyo inayohusika na usajili wa vijiji, lakini kutokana na matatizo yaliyojitokeza kwenye migogoro hii ya vijiji 975, kuanzia sasa hatutasajili tena kijiji mpaka tuwasiliane na sekta na wizara zingine,” alisema.

Silinde alisema kutoshirikisha wadau muhimu wakati wa kusajili vijiji, kumesababisha kuwapo vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi, hivyo kuchangia migogoro ya matumizi ya ardhi.

Wakati wa kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Kamati ya Mawaziri inayoongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ilibaini baadhi ya vijiji kusajiliwa ndani ya mipaka ya hifadhi na kuwa na miundombinu ya kijamii.

Akielezea utekelezaji wa uamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975, Waziri Lukuvi alisema mkoa wa Tabora unahusisha vijiji 100 na ni mkoa wenye vijiji vingi kulinganisha na mikoa mingine. Alisema vijiji 94 kati ya hivyo ndivyo vitakavyobaki na maeneo yake kama yalivyo.

Kwa mujibu wa Lukuvi, mchanganuo wa utekelezaji uamuzi wa Baraza la Mawaziri ni kuwa vijiji 50 vilivyosajiliwa ndani ya hifadhi vitaendelea na hadhi yake huku vijiji 15 migogoro yake ikiwa tayari imetatuliwa na kijiji kimoja vitongoji vyake vitabaki kwenye hifadhi.

Aidha, alisema kuna vijiji 11 vitakavyomegewa maeneo katika hifadhi na vijiji 17 vilivyokuwa na migogoro ya mipaka na hifadhi vitabaki lakini mipaka yake itarejewa kwa njia shirikishi.

‘’Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza tutekeleze uamuzi huu kwa umakini mkubwa bila ya kuleta taharuki kwa wananchi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla,’’ alisema Lukuvi.

Habari Kubwa