Mazembe na majembe yote waja kuivaa Simba

26Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mazembe na majembe yote waja kuivaa Simba
  • ***Simba Super Cup kunoga, Jembe lingine latua Msimbazi, Al Hilal nao waleta nyota wanaoitesa Al-Merrikh kule Sudan huku...

MABINGWA wa zamani wa Afrika, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Al Hilal ya Sudan zinatarajiwa kuwasili nchini leo zikiwa na 'majembe' yao ya vikosi vya kwanza kwa ajili ya kushiriki mashindano maalum ya Simba Super Cup yatakayoanza kesho jijini Dar es Salam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema maandalizi ya mashindano hayo ya kwanza yamekamilika na wageni wao watakuja wakiwa na nyota wao muhimu wa kikosi cha kwanza kwa kila moja ikiwa na lengo la kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Barbara alisema Simba pamoja na timu hizo mbili zimejiandaa kuonyesha burudani safi pamoja na kujiimarisha kuelekea mechi za hatua ya makundi kupitia mashindano hayo.

"Timu zote mbili zinawasili kesho (leo), TP Mazembe inakuja na mastaa wake wote muhimu kama nyota Kalaba (Rainford), tunatarajia mashindano haya yatatusaidia kiufundi na kwetu kocha atapata nafasi ya kuwaona wachezaji wake na kutengeneza mfumo atakaokuwa anautumia," alisema Barbara.

Wachezaji wa TP Mazembe ambao wametangazwa kuwa watakuwamo katika kikosi hicho mbali na Kalaba ni; Sylvain Gbohou, Patou Kabangu, Moukoro Bosso, Mputu Mabi Tresor, Thomas Ulimwengu, Moustapha Kouyate, Koffi Kouyate, Bakula Ulonde na Martial Zembe Ikoung.

Wengine ni Mayombo Etienne, Ochaya Benson, Mwape Tandi, Kabaso Chngo, Okito Kazadi Nicolas, Gmasengo Yumba Godet, Bossou Nzali Adam, Kisangala Boba, Sudi Bibonge, Tshibangu Isaac, Joel Freddy Kaougi, Bedi Guy Stephane, Binemo Madi Le Beau na Arsene Zola Kiaku.

Kuhusu michuano hiyo ya Simba Super Cup, Barbara aliongeza kuwa itakuwa ya kila mwaka na klabu hiyo itaendelea kuitafutia muda sahihi wa kufanyika ili iwe bora zaidi kiufundi kwa timu zote zitakazoshiriki.

"Kwa mfano mwaka huu tulitamani tuiweka Namungo kwa sababu nao wanashiriki mashindano ya kimataifa, lakini muda uliopo ni mdogo, nao ingewasaidia kuwaimarisha na huko mbele tunafikiria pia kuwaalika Yanga, tutawaandikia barua rasmi ya kuwajulisha," Barbara alisema.

Aliongeza kanuni za mashindano hayo zitatangazwa leo baada ya kufanyiwa kazi na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wanawashukuru wageni wao TP Mazembe na Al Hilal kwa kuthibitisha kushiriki michuano hiyo.

Mechi ya kwanza ya ufunguzi ya michuano hii itachezwa kesho kati ya wenyeji Simba dhidi ya Al Hilal na Januari 29, mwaka huu TP Mazembe watawakabili Wasudan hao na mchezo wa mwisho utawakutanisha Simba dhidi ya Mazembe Januari 31, mwaka huu.

Aidha, Barbara alisema baada ya michuano hiyo Simba itasafiri kuelekea jijini Dodoma tayari kwa ajili ya mechi yao ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji itakayopigwa Februari 4, kabla ya siku tatu baadaye kucheza kiporo kingine katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. 

Katika hatua nyingine klabu ya Simba jana imemtambulisha straika wake mpya, Mnigeria Junior Lokosa.

Katika ukurasa wake wa kijamii, Simba imesema lengo kuu la kumsajili mchezaji huyo ni kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini lengo mama likiwa ni kutwaa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, huku ikimwelezea kuwa ni straika hatari, ambaye aliwahi kuichezea timu ya Esperance ya Tunisia na ataanza kuonekana kwenye michuano ya Simba Super Cup.

Habari Kubwa