Msichana aongoza shindano la Hisabati na Sayansi

28May 2019
Enock Charles
DAR
Nipashe
Msichana aongoza shindano la Hisabati na Sayansi

MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam, Salma Sadiki, ameongoza shindano la masomo ya Hisabati na Sayansi yaliyoshirikisha zaidi ya wanafunzi 340.

Mkuu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Hazina, Dennis Nyakerandi (kushoto), akikabidhi zawadi ya vitabu kwa mwanafunzi wa shule hiyo, Salma Mushi, aliyeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Hisabati na Sayansi, yalifanyika katika Shule ya Feza, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kushirikisha wanafunzi zaidi ya 350 kutoka shule mbalimbali. Wengine ni wanafunzi wa shule hiyo, waliofanikiwa kuingia 10 bora katika mashindano hayo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Mashindano hayo yaliandaliwa mwishoni mwa wiki na shule za Feza na kushirikisha shule mbalimbali za msingi za umma na za binafsi jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa taaluma wa shule hiyo, Dennis Nyakerandi, alisema mwanafunzi huyo alipewa zawadi ya cheti na Sh. 300,000.

Aliwataja wanafunzi wengine wa Hazina walioingia 10 bora kwenye mashindano hayo kuwa ni Ibrahim Sharif aliyeshika nafasi ya pili na nafasi ya nne ilichukuliwa na Patricia Benatus wa shule hiyo.

Aliwataja wengine kuwa ni Sahill Imam, aliyeshika nafasi ya tano, Maliki Yassin, nafasi ya sita na nafasi ya nane ilichukuliwa na Khaulat Majid wa shule hiyo ya Hazina.

Denis alisema matokeo hayo yamewapa motisha kwamba wanaendelea kufanya vizuri kwenye taaluma na wanatarajia kufanya vizuri zaidi kwenye mitihani inayokuja.

"Ushindi huu haukuja tu umetokana na jitihada za walimu kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya mitihani, hivyo sisi imetupa moyo kwamba kazi tunayofanya inazaa matunda," alisema.

Alisema kwenye mashindano hayo wanafunzi walifanya mtihani wa Hisabati na Sayansi na walipaswa kumaliza ndani ya saa mbili.

Habari Kubwa