Msigwa amwangukia Kinana

20May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Msigwa amwangukia Kinana

MBUNGE wa Iringa Mjini, amemwomba radhi Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na kauli za uongo alizowahi kuzitoa dhidi yake.

Katika nyakati tofauti, ndani na nje ya Bunge, Mchungaji Peter Msigwa aliwahi kutoa kauli za uzushi dhidi ya Kinana, akimtuhumu kujihusisha na ujangili na biashara ya nyara za serikali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema tuhuma zote alizowahi kuzitoa dhidi ya Kinana bungeni na kwenye mikutano ya kisiasa nje ya Bunge, hazikuwa na ukweli wala ushahidi wowote.

“Ni dhahiri kwamba nimemkosea, nimemdhalilisha na kumkashifu ndugu yangu Abdulrahman Kinana. Nimekutana na kuzungumza naye kuhusu jambo hili na kumwomba radhi. Ninashukuru kwamba amekubali kunisamehe.

“Bila shaka mtakubaliana nami kwamba Kinana ni mzalendo, muungwana na mstaarabu ambaye kwa kweli hastahili kukashifiwa wala kudhalilishwa. "Nitaendelea kumheshimu kama alivyodhihirisha ustahimilivu na uungwana wake kwangu, kwa familia yangu na kwa Watanzania," Mchungaji Msigwa alisema.

Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia kesi namba 108 ya mwaka 2013, ilimkuta Mchungaji Msigwa na hatia ya kuandaa na kutoa kashfa dhidi ya Kinana kwa malengo ya kisiasa, kumchafulia jina na kumshushia hadhi yake katika jamii; ndani na nje ya nchi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mchungaji Msigwa alisema kujutia kitendo chake hicho kwa kusema yeye ni binadamu na kukosea ni jambo la kawaida na kilichofanywa na Kinana kwenda kumshtaki mahakamani ni jambo la haki.

“Ninakiri mbele yenu kwamba tuhuma nilizozitoa mara kwa mara dhidi ya Ndugu Kinana hazikuwa na ukweli wala ushahidi wowote. Taarifa nilizopewa na kuzitumia hazikuwa zimefanyiwa utafiti, bali za kuungwaungwa na zenye malengo ya kisiasa na kizandiki.

“Hata hivyo, mambo kama haya hutokea katika maisha na sisi kama binadamu hutokea tukawakosea wenzetu. Inapotokea kuwakosea wenzetu, tunatakiwa kuwa tayari kuomba radhi na tunaowakosea nao kuwa tayari kusamehe,” alisema.

Kabla ya kupeleka suala hilo mahakamani, Kinana kupitia kwa Wakili wake, Erick Sikujua Ng’maryo, alimtaka Mchungaji Msigwa kufuta kauli zake hizo na kuomba radhi hadharani kwa kuwa hazikuwa na ukweli wowote.

Mbunge huyo alikataa kufanya hivyo na kusema yuko tayari kujitetea mahakamani. Jaji Zainab Muruke aliyesikiliza na kuamua kesi hiyo, alisema kitendo cha wanasiasa kutoa kauli za kudhalilisha wenzao pasipo kuwa na ushahidi wala ukweli wowote ni “tabia mbaya” inayopaswa kukemewa.

“Kumekuwa na dhana kwamba siasa ni mchezo mchafu na kwamba kauli za kudhalilisha heshima na utu wa wengine zinakubalika kwenye majukwaa ya kisiasa.

Hii si sahihi kwa sababu wanasiasa na viongozi wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa mbele ya jamii.

“Katika kutoa hukumu, Mahakama Kuu imetambua historia ya uongozi na utendaji uliotukuka wa Ndugu Kinana ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu ikiwa ni pamoja na ubunge, uwaziri, Uspika wa Bunge la Afrika Mashariki, Ukatibu Mkuu wa CCM na majukumu mengine ya kiuongozi katika ukanda wetu huu na kimataifa.

“Imedhihirika wakati wa kusikilizwa kesi hii na kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, tuhuma dhidi ya Kinana zilikuwa na lengo la kumchafua, kumdhalilisha na kumshushia heshima katika ngazi zake za kiuongozi na bila shaka zikiwa na msukumo wa kisiasa,” Jaji huyo alisema.

Kesi hiyo ilinguruma Mahakama Kuu kwa miezi 36 kabla ya kutolewa hukumu, huku shauri lenyewe likisikilizwa mahakamani mara 84. Mchungaji Msigwa hakuwahi kufika mahakamani wala kuwasilisha mashahidi katika kesi hiyo aliyokuwa akitetewa na Wakili Peter Kibatala katika hatua za awali na baadaye Hekima Mwasepo.

Habari Kubwa