Muswada kubana ndege zisizo na rubani wapelekwa bungeni

14Feb 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Muswada kubana ndege zisizo na rubani wapelekwa bungeni
  • *Wazee wa mahakama kuondolewa

SERIKALI imewasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine, unalenga kuzibana kurusha ndege zisizo na rubani kutokana na sababu za kiusalama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge jana, muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, katika Sheria ya Usafiri wa Anga, wanapendekeza kuipa Mamlaka ya Usafiri wa Anga uwezo wa kuzuia ndege zisizo na rubani kuruka bila kibali maalum.

“Pia, inapendekezwa kuipa uwezo mamlaka kuingia makubaliano ya kiutendaji na mamlaka za nchi nyingine ili kuiwezesha mamlaka kuruhusu nchi hiyo kufanya ukaguzi kwa ndege za Tanzania zinazofanya biashara na nchi hiyo au nchi nyingine inayofanya biashara na Tanzania," alisema.

Kuhusu Sheria ya Mawakili, alisema inalenga kuanzisha Kamati za Maadili za Mawakili kwa ngazi ya mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa haki.

“Pia, kumwezesha mwananchi anayemlalamikia wakili kwa ukiukaji wa maadili kushughulikia tatizo lake katika ngazi ya mkoa bila ya uhitaji wa kusafiri kuifuata kamati ya maadili katika ngazi ya taifa," alisema.

Kwenye Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, muswada huo unapendekeza ubadilishanaji wa taarifa za usajili wa matukio muhimu baina ya taasisi moja na nyingine.

Kuhusu Sheria ya Majina ya Biashara, muswada unapendekeza majina ya biashara yanayosajiliwa yawe ni ya wale tu wanaokidhi vigezo vya kusajiliwa kwa madhumuni mahsusi.

Pia inapendekezwa kuongeza adhabu ya faini ili kuhakikisha adhabu inayotolewa na sheria inaendana na wakati na hivyo kuzuia utendaji wa makosa.

Katika Sheria ya Kampuni, muswada unapendekeza kuhakikisha watu wenye sifa ya kusajili kampuni ni wale tu wenye sifa na watapaswa kuwasilisha taarifa zao binafsi.

Pia, unapendekeza kuweka katazo au zuio la kusajili kampuni kwa watu waliowahi kutiwa hatiani au ambao taarifa zao zimetolewa na mamlaka husika kuwa mwombaji wamekuwa wakijihusisha na makosa yanayohusiana na utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi, biashara ya binadamu, biashara ya dawa za kulevya au makosa mengine yanayohusiana nayo.

Inapendekezwa katika muswada huo kuruhusu watu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 kuteuliwa kuwa wakurugenzi wa kampuni.

Kwenye Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, inapendekezwa kubadilisha muhula wa kushikilia nafasi kwa wenyeviti wa mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.

Muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mahakama za Mahakimu ili kuwaondoa wazee washauri wa mahakama katika mahakama za mwanzo kwa kuwa mahakama hizo sasa zinasimamiwa na mahakimu wakazi wenye weledi wa sheria na hivyo kuongeza kasi ya utoaji haki kwa wakati...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa