NEC: Atakayejitangaza mshindi atashughulikiwa

21Oct 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
NEC: Atakayejitangaza mshindi atashughulikiwa
  • *Orodha ya mawakala yahitajika leo

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kikundi, taasisi, chama cha siasa au mtu yeyote atakayetangaza matokeo ya uchaguzi mkuu kwa ngazi yoyote kabla ya mamlaka, atachukuliwa hatua stahiki.

Vilevile, imevikumbusha vyama vya siasa kuhakikisha vinawasilisha orodha na barua za utambulisho wa mawakala wa vyama kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo husika.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu wajibu wa vyama vya siasa na wagombea wakati wa kampeni, uteuzi na mamlaka ya vyama vya siasa na utangazaji wa matokeo.

Alisema NEC inakumbusha kuwa mamlaka za kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais, ubunge na udiwani ni ya tume.

"Kwa msingi huu, atakayefanya hivyo kabla ya mamlaka rasmi zilizowekwa kikatiba na kisheria, atakuwa amevunja sheria na hatua stahiki za kisheria zitapaswa kuchukuliwa dhidi yake," alionya.

Jaji Kaijage alisema tume haitarajii kuona kikundi, taasisi, chama cha siasa, wagombea na wafuasi wao au mtu yeyote akijichukulia sheria mikononi kutangaza matokeo ya uchaguzi nje ya utaratibu na mamlaka zilizowekwa kikatiba.

Katika mkutano wake huo, Jaji Kaijage pia alisema NEC inavipongeza vyama vya siasa na wagombea ambao wanaendelea na kampeni kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi.

Habari Kubwa