Nyumba ya Nyerere yapata maji kwa mara ya kwanza

14Feb 2021
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Nyumba ya Nyerere yapata maji kwa mara ya kwanza

NYUMBA aliyokuwa anaishi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, miaka 58 iliyopita katika eneo la Shule ya Sekondari Pugu jijini Dar es Salaam, jana ilipata maji kwa mara ya kwanza baada ya huduma hiyo kufikishwa kwenye eneo hilo.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, jana alizindua njia ya maji katika nyumba hiyo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa maji Kisarawe-Pugu-Gongo la Mboto ambao unatekekezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kwa gharama ya Sh. bilioni 6.9.

Alisema Mwalimu Nyerere alikuwa akiishi kwa miaka 58 iliyopita na kipindi chote hapakuwa na maji hadi jana alipozindua huduma hiyo.

"Kama serikali tungefurahi sana kama leo mzee wetu angekuwapo kwenye nyumba hiyo, tukamzindulia maji akayaona yanatoka.

Ni ukweli usiojificha kuwa tumechelewa sana, lakini tumefanya, ni fahari yetu kwamba nyumba hii ya kihistoria tumekuja kufungua njia ya maji kwa Dar es Salaam Kusini kutoka hapa kwenye nyumba ya kihistoria.

"Sisi inatupa faraja kuwa maagizo ya Baba wa Taifa, maagizo ya mwasisi wetu tumeyafanyia kazi na leo tumefanya ushahidi na Watanzania wanaona na ni imani yetu na hili tunalolifanya, naye anaendelea kupumzika salama huko aliko," alisema.

Samia alisema watafanya ziara za mara kwa mara kufuatilia kama maagizo wanayoyatoa yanafanyiwa kazi.

Alisema watakapokwenda kuzindua wiki ya maji, watanzunguka Tanzania yote kwenye miradi ya maji kwa lengo la kuangalia kazi walizowapa kama zimetekelezwa.

"Ziara nilivyofanya ya Bagamoyo, ilikuwa na maneno maneno kidogo. Kwanini Makamu wa Rais ameruka Mkoa wa Dar es Salaam wakati hatuna maji, lakini DAWASA walijipanga, hivyo tuanzie huko na baadaye nije Dar es Salaam kwa sababu huko ndiko kuna chanzo kikubwa cha maji," alisema.

Alisema takwimu za Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ilala zinaonyesha maeneo ya Ukonga, Segerea na maeneo yao kuna maradhi makubwa yatokanayo na ukosefu wa majisafi na salama, hivyo kupatikana kwa maji hayo kunakwenda kupunguza wimbi la maradhi hayo kwa wananchi.

Alisema DAWASA wamefanya kazi nzuri katika mradi huo kwa gharama ambazo zinakubalika na mwelekeo wa serikali ni kupunguza gharama za utekekezaji wa miradi ya maji.

Samia alisema mamlaka hiyo imeahidi kuwa watakapotoka madarakani mwaka 2025, Dar es Salaam itakuwa imepata maji kwa asilimia 100 na hakuna ambaye atakosa maji jijini humo.

Samia aliwataka wananchi kuacha mchezo wa kuharibu miundombinu ya maji kwa kuwa serikali inatumia gharama kubwa katika kuwawekea maji, hivyo ni vizuri wakawa wazalendo katika kuilinda.

Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange, alisema tangu mamlaka hiyo ilipoanzishwa, matokeo yake ni mazuri na wamejipanga upya kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa na midogo.

"Siyo maji yanatoka mara moja kwa wiki, tunataka tuhakikishe huduma ya maji inapatikana kila wakati kwa saa 24, huo ndiyo mkakati wetu," alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Cyprian Luhemeja, alisema mamlaka hiyo imejipanga kutekeleza miradi yake kwa kutumia fedha zao kwa kuwa walipewa maelekezo na wizara kutumia asilimia 35 ya mapato yao katika miradi.

Alisema mradi wa Ukonga ni mkombozi kwa wananchi kwa sababu walikuwa wanapata shida ya maji, akitamba kuwa kata zote zitapata maji na ifikapo Desemba mwaka huu, maji yatapatika kwa asilimia 100 kwa mkoa mzima.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, alisema Sh. trilioni moja zimewekezwa kwenye miradi ya maji kwa mkoa huo na tatizo la maji litakuwa ni historia.

Habari Kubwa