Okwi, Chama wamfariji Mo

22Oct 2018
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Okwi, Chama wamfariji Mo
  • ***Waipeleka Simba hadi nafasi ya tatu kwa kuizabua Stand United mabao....

SIKU moja baada ya mfadhili na mwekezaji mtarajiwa wa Simba Mohammed "Mo" Dewji, kupatikana, wachezaji wa timu hiyo wamekoleza furaha ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuiwezesha kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United jana.

mshabuliaji wa simba EmManuel OKWI PICHA NA MTANDAO

Kiungo fundi wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi ndiyo walioongoza faraja hiyo kwa Mo baada ya kuiibuka mashujaa wa timu hiyo kwa kufunga mabao mawili huku goli la tatu likitokana na beki wa Stand United kujifunga kufuata kona iliyochongwa na Shiza Kichuya.

Simba iliandika bao la kwanza kupitia kwa Chama dakika ya 31 kufuatia shambulizi la maana lililofanywa na timu hiyo. Baada ya kupata bao hilo, Simba waliendelea kulishambulia lango la Stand kama nyuki huku ikimjaribu zaidi kipa wa wapinzani wao hao kwa mikwaju ya mbali.

Wakati mwamuzi msaidizi akionyesha zimebaki dakika mbili kabla ya mapumziko, Okwi alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ndefu na kumchambua golikipa wa Stand United, Mohamed Mandanda. Simba waliendelea kulisakama lango la Stand huku kipindi cha pili wakiongeza kasi na kufanya mashambulizi mfululizo.

Dakika ya 77, mpira wa kona uliopigwa na Kichuya uligongwa kichwa na beki wa Stand aliyekuwa akijitahidi kuucheza usimfikia Meddie Kagere, lakini ulielekea langoni kwao na kusindikizwa na nyavuni golikipa Mandanda. Simba wangeweza kuibuka na ushindi mnono zaidi kama Mohammed Ibrahim angetumia vyema nafasi aliyoipata dakika 67 baada ya kupiga shuti lilozuiliwa na beki wa Stand na kuwa kona tasa.

Simba iliendelea kumiliki mpira na kutawala mchezo kwa nafasi kubwa huku wakishindwa kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza.

Ushindi huo wa jana unaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya tatu kufuatia kufikisha pointi 17 baada ya kucheza michezo nane huku ikilipa ushindi wa juzi wa Yanga wa mabao 3-0 dhidi ya Alliance ya Mwanza.

Azam FC iliyoshuka dimbani mara tisa ipo kileleni ikiwa na pointi 21, wakati Yanga iliyocheza mechi saba hadi sasa ikiwa nafasi ya pili na pointi 19 kibindoni.

Simba kwa sasa ipo katika kipindi cha furaha kubwa kufuatia Mo aliyetekwa kwa muda siku tisa na watu wasiojulikana kabla ya Ijumaa usiku kupatikana maeneo ya Gymkhana jijini Dar es Salaam akiwa ametelekezwa, jambo ambalo lilizua hofu kubwa kwa wanachama wa Simba, mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla.

Kabla ya mechi hiyo ya jana, wachezaji waliahidi kumpa furaha Mo kwa kuibuka na ushindi jambo ambalo wamelitekeleza kwa vitendo Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa