Pinda ataka miti milioni moja kila halmashauri

17Oct 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Pinda ataka miti milioni moja kila halmashauri

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kupanda miti milioni moja kila moja katika utekelezaji wa kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

Pinda alitoa rai hiyo jana alipoongoza upandaji miti katika Shule ya Sekondari Nala jijini hapa ulioratibiwa na Taasisi ya Habari Development.

Alisema uwapo wa miti utasaidia kuimarisha mazingira ya maeneo hayo ili kuondoa dhana ya kuwa Dodoma ni kame.

Alisema Makao Makuu lazima pawe pa kijani kwa kupanda miti kwa wingi ili kuwa na mazingira bora.

Alihimiza  miti hiyo itunzwe ili isife kwa kukosa matunzo.

Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, aliishukuru taasisi hiyo kwa jitihada za kuimarisha mazingira mkoani Dodoma.

Mavunde alisema kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha Dodoma inakuwa ya kijani kama ilivyo mikoa mingine nchini huku akiahidi kuunga mkono kampeni mbalimbali za kuboresha mazingira ya Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, alisema faida ya kupanda miti shuleni ni pamoja na kutoa maarifa bora kwa wanafunzi.

Alisema ni muhimu maeneo ya shule kuwa na miti ambayo wanafunzi watajifunza kupitia vivuli vya miti hiyo kwa kujisomea.

"Hivyo miti ni muhimu sana katika jamii hususani shuleni ambapo mazingira yenye miti yana faida kubwa sana kwa wanafunzi," alisifu.

Awali, Katibu wa Taasisi hiyo, Bernad James, alisema miti walioipanda katika shule hiyo inapaswa kuwa mfano katika kata hiyo ili kuhakikisha wanaifanya Dodoma kuwa ya kijani.

Alisema miche ya miti 700 walioipanda wanahitaji kuona yote inatunzwa ili eneo liwe la kijani.

"Tunaomba uongozi wa shule uwe mfano wa utunzaji miti, mnatakiwa kuwa mfano katika shule hii," alisema.

Habari Kubwa