Polisi wathibitisha kumshikilia Mbowe

22Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi wathibitisha kumshikilia Mbowe

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limethibitisha kumshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa mahojiano kutokana na kuandaa mikusanyiko isyokuwa na kibali.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi amesema kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia jana Jumatano Julai 21 akiwa hoteli ya Kingdom mtaa wa Ghana alikokifikia.

"Baada ya kumkamata, wenzetu wa Dar es Salaam nao walitueleza kuwa wanamtafuta kwa makosa mengine anayodaiwa kuyafanya huko, hivyo tulimsafirisha kwenda Dar es Salaam anakoendelea kuhojiwa," amesema.

Amesema kiongozi huyo wa Chadema hivi sasa yuko kwenye mikono salama ya polisi Mkoa wa Dar es Salaam na atarejeshwa Mwanza baada ya mahojiano ili aunganishwe na wenzake 15 wanaoshikoliwa kuhusiana na kongamano la Katiba Mpya lililozuiwa na jeshi hilo jana.

Mratibu wa uhamasishaji wa Baraza la Vijaana wa Chama hicho, Twaha Mwaipaya, kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter ameandika kuwa jeshi la polisi asubuhu ya leo liliwakusanya watuhumiwa wote wa Kongamano la Katiba sehemu moja kwaajili ya mahojiano, Ila Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Pambalu pamoja na Mjumbe wa Halmshauri Kuu John Heche wamechukuliwa wamechukuliwa kituoni hapo na haijulikani wamepelekwa wapi.

Habari Kubwa