Raia China watuhumiwa kumpa Kamishna TRA mlungula mil. 11/-

26Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Raia China watuhumiwa kumpa Kamishna TRA mlungula mil. 11/-

RAIA wawili wa China wanaodaiwa kuwa mke na mume, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na tuhuma za kutoa rushwa ya Sh. milioni 11.5 kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Edwin Mhede.

Washtakiwa hao, Zheng Rongnan (50) na Ou Ya (47), wote wakazi wa Kinyambo, Mafinga C, Iringa wamefikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huduma Shaidi.

Wakili wa Serikali, Mwakatobe Mshana, alidai kuwa Februari 24, mwaka huu, washtakiwa wote wakiwa katika Makao Makuu ya TRA yaliyopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, walitoa rushwa ya Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 11.5) kwa Kamishna Mkuu Dk. Mhede, kama kishawishi cha kuwasaidia kampuni yao isilipe kodi ya Sh. bilioni 1.3 kiasi ambacho kilipaswa kuilipa mamlaka hiyo.

Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo. Hakimu Shaidi alisema kufuatia washtakiwa kukiri kosa hilo, kesi hiyo italetwa leo kwa ajili ya maelezo ya awali na upande wa mashtaka umlete mkalimani kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza ambaye hajui Kiingereza.

Habari Kubwa