Rais Samia hatabiriki

01May 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Rais Samia hatabiriki

HATABIRIKI! Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuibuka na sura mpya kwenye Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kama ilivyokuwa katika kupendekeza jina la Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, na uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, jana Rais aliibuka na majina yasiyotarajiwa ya makada wa CCM wanaochukua nafasi ya Katibu Mkuu na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho.

Muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM na kuuhutubia mkutano mkuu wa chama hicho jijini Dodoma, Halmashauri Kuu Maalum (NEC), ilimpitisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Bashiru Ally.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kikao hicho cha NEC jana, aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alisema kikao hicho chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia, imeridhia kwa kauli moja Sekretarieri mpya ya chama hicho iongozwe na Chongolo.

“Kikao hiki maalum kimeitishwa na Mwenyekiti wetu mpya na kazi ilikuwa moja,  kuitizama sekretarieti ambayo ndiyo chombo cha utendaji kwa sababu kila tunapopata mwenyekiti mpya huwa tunapata watenda kazi,”alisema.

Polepole alisema kazi ya msingi ilikuwa ni kuitangaza sekretarieti na kujaza nafasi na kupanga safu ya uongozi katika chama.

“Kama mnavyojua ndani ya chama mtu mmoja kofia moja, kama mnavyojua mimi viongozi wa chama walinipeleka kuwa mbunge na Mwenyekiti wa Bunge kusukuma kazi ya chama kule, hivyo nafasi yangu itachukuliwa na Shaka Hamdu Shaka, kama mnavyojua ana uzoefu mkubwa ndani ya chama,” alisema.

Wajumbe wengine wa sekretarieti ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Zanzibar anaendelea na nafasi yake Abdallah Mabodi huku Tanzania Bara akiteuliwa Christina Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, akichukua nafasi ya Rodrick Mpogolo ambaye atapangiwa majukumu mengine ya kitaifa.

Pia, Makatibu wa NEC wanaoshughulikia Fedha na Uchumi (Frank Hawasi), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Ngemela Lubinga), Oganaizesheni (Maudline Castico) anachukua nafasi ya Pereira Silima ambaye pia atapangiwa majukumu mengine.

Habari Kubwa