RC aonya vijana vurugu uchaguzi

25Oct 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
RC aonya vijana vurugu uchaguzi

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, amewataka vijana mkoani hapa kuacha kurubuniwa na baadhi ya wanasiasa kufanya fujo wakati wa uchaguzi mkuu wa Jumatano.

Alitoa onyo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Telack alisema kuna tetesi kuhusu baadhi ya vijana kutaka kufanya fujo siku hiyo ya uchaguzi mkuu, akiwataka waache kwa kuwa serikali imejipanga vyema kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.

"Tarehe 28 mwezi huu ambayo ni siku ya Jumatano, tutakuwa na uchaguzi mkuu, hivyo nitoe tahadhari kwa vijana, wasirubunike kufanya fujo zozote zile, tutawashughulikia, tunataka uchaguzi umalizike kwa amani.

"Amani hii tuliyonayo nchini, mataifa mengi yanatamani ivurugike, na sisi hatutakubali, mtu ukishindwa, kubali matokeo, uchaguzi ni kama mpira, ukifungwa goli, jipange mchezo ujao," alisema.

Kiongozi huyo alisema wameshatoa maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi kuwa watu wenye uhitaji maalum wakiwamo wazee, wajawazito na wenye watoto wadogo, wapewe kipaumbele kuanza kupiga kura na siyo kujipanga mstari.

Telack pia aliwaonya waandishi wa habari kuhusu kujihusisha na utangazaji wa matokeo kwenye vituo vya kupigia kura, akisisitiza kuwa kazi hiyo ni ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika.

Alisema waandishi wa habari hawapaswi kutangaza matokeo ambayo msimamizi hajayatangaza, ili wasilete taharuki.

Habari Kubwa