Ripoti Maalum: Kipato chakwamisha wazazi kununulia wanafunzi barakoa

06Jul 2020
Zuwena Shame
Singida
Nipashe
Ripoti Maalum: Kipato chakwamisha wazazi kununulia wanafunzi barakoa

KIPATO kidogo kimesababisha changamoto kwa wazazi wengi kushindwa kuwanunulia watoto wao barakoa katika Kijiji cha New Kiomboi, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Luzilukulu, Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, wakiwa kwenye viwanja vya shule hiyo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe wilayani humo katika shule za msingi na sekondari, umebaini kuwa tangu shule zifunguliwe Juni 29, watoto wengi wanahudhuria shuleni bila kuvaa barakoa.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa mwongozo unaowataka wanafunzi kuanzia miaka miaka minane na wasio na matatizo ya kiafya kuvaa barakoa wanapokuwa shuleni.

Katika Shule ya Msingi ya Igumo, Kijiji cha New Kiomboi, siku ya kwanza ya kuripoti shule ni mtoto mmoja pekee aliyekuwa amevaa barakoa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Edward Mlundi, alisema uvaaji barakoa ni changamoto kwa watoto wengi shuleni hapo kutokana na wazazi wengi kuwa na kipato duni.

“Wazazi wengi wanaona kumnunulia mtoto barakoa ni gharama na kuona bora kutumia hela hiyo kwa shughuli zingine,” alisema.

Mlundi alisema siku ya kwanza shule zilipofunguliwa ni mwanafunzi mmoja pekee aliyevaa barakoa na wenzake walimdhihaki kwa kumcheka.

Hata hivyo, Mwalimu Mlundi alisema aliwaelimisha wanafunzi hao umuhimu wa kuwaambia wazazi wao wawanunulie barakoa.

Alisema siku ya pili mwitikio ulikuwa mzuri na idadi ikafikia wanafunzi watatu.

"Hii changamoto ni kuwa wazazi huku vijijini hawana uwezo wa kumudu kununua barakoa kwa ajili ya kuwakinga watoto wao na janga la corona," alisema. Mwalimu Mlundi.

Kuhusu utaratibu wa kuwa na chakula shuleni baada ya muda wa masomo kuongezwa shuleni, Mlundi alisema kuwa kwa sasa bado utaratibu huo haujawekwa sawa kwa sababu likizo ya corona imeleta athari na chakula kilichokuwapo shuleni kama unga wa mahindi na maharage vimeharibika.

Aliongeza kuwa shule ipo katika mchakato wa kutayarisha chakula kilichokuwa stoo ili kutatua changamoto hiyo kwa kuwa hata wanafunzi wa shule ya awali wameshindwa kupata lishe ya uji.

Lailat Amis (10) mwanafunzi wa shule ya Igumo wilayani humo alisema wamepewa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa wa corona kama kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa, lakini mzazi wake hajamnunulia kwa sababu hana uwezo huo.

Lailat alisema kuwa anatamani na yeye angekuwa na uwezo wa kuvaa barakoa kama wengine kwa kuwa ni njia ya kujikinga na corona.

Katika Shule ya Msingi Kigeza TANESCO, ambayo ni shule yenye watoto wenye uhitaji maalumu kama wenye uono hafifu, wenye ualbino na ulemavu wa viungo ni watatu pekee waliokuwa na barakoa shuleni.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Andrea Muna, alisema wazazi walipata taarifa kuhusu wanafunzi kuvaa barakoa, lakini mwamko ni mdogo sana hasa ikizingatiwa kipato cha wengi kuwa duni.

Muna alisema pia wazazi hawaoni umuhimu wa kuwapa watoto barakoa kwa sababu hulka ya kusema kuwa katika maeneo wanayoishi hakuna mgonjwa au hata mtu ambaye amefariki kwa ugonjwa huo.

Alisema, uongozi wa shule umejitahidi kwa kuweka ndoo za maji na sabuni kuzunguka shule na hata kwenye mabweni ya wanafunzi ili kujikinga na ugonjwa huo.

Kuhusu suala la chakula kwa watoto shuleni hapo, alisema wa kutwa wanarudi nyumbani kula na kurudi shule, lakini wenye mahitaji maalumu wanakula shuleni.

Pili Salaganda (15), mwanafunzi wa darasa la saba, alisema elimu juu ya kujikinga na ugonjwa wa corona imetolewa vizuri shuleni, changamoto kwao ni barakoa kutokana na mzazi wake kutomnunulia.

Salaganda alisema kuwa mzazi wake hana uwezo wa kumnunulia barakoa na hivyo anajikinga kwa kunawa mikono na maji tiririka na sabuni kwa kuwa shule yao ina vifaa vya kutosha.

Naye Ezekiel Kikwezi (14), akizungumzia likizo ya corona, alisema alikuwa anamsaidia mzazi wake kufanya kazi za nyumbani na kumkwamisha kimasomo kwa kuwa waliporejea shule walianza kurudi nyuma kimasomo.

Akizungumzia uvaaji barakoa alisema atambeleza mama yake amnunulie ili ajikinge na ugonjwa wa Covid-19.

"Najua umuhimu wa kuvaa barakoa, nitambeleza mama yangu aninunulie barakoa na mimi nijikinge," alisema.

Katika Shule ya Sekondari New Kiomboi, yenye idadi ya wanafunzi 595 hakuna aliyevaa barakoa.

Kuhusu suala hilo la wanafunzi kutovaa barakoa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Amadeus Kiduu, alisema changamoto hiyo imetokana na mwitikio hasi kwa wazazi wengi kutowanunulia watatoto wao.

Alisema uongozi wa shule unaendelea kuhamasisha wanafunzi kuwaambia wazazi wao umuhimu wa kuvaa barakoa.

Kuhusu wanafunzi wengi kukaa kwenye darasa moja, alisema changamoto ni uchache wa miundombinu ya madarasa.

Alisema kuna madarasa 11 ambayo hayajitoshelezi kuwatenganisha wanafunzi kwa kanuni ya mita moja kama njia moja wapo ya kujikinga na corona.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto za shule za msingi, Ofisa Elimu (msingi), Chacha Kehogo, alisema wazazi wengi kipato chao ni duni na hawana uwezo wa kununua barakoa kwa ajili ya watoto wao hasa za kiuuguzi hivyo wanashauri wazazi wawashonee watoto za vitambaa ili kuwakinga watoto na corona.

Alisema pia ni jitihada kubwa kwa sasa ni kuwakinga watoto kwa maji tiririka na sabuni ili waweze kuendelea na masomo yao.

Kuhusu kuongezeka saa za kujisomea, Kehogo alisema kwa sasa ofisi yake ina mkakati wa kuhamasisha walimu kujitolea kufundisha wanafunzi siku za Jumamosi ili kukimbizana na silabasi za masomo hasa kwa wanafunzi wa darasa la nne na la saba ambao wanakabiliwa na mitihani yao ya kitaifa.

Vile vile, suala la kukaa mita moja, Kehogo alisema madarasa ni machache na wameshauri kuwa na zamu mbili za kuingia darasani kwa wanafunzi wa shule za msingi wote isipokuwa shule za awali.

Naye Ofisa Elimu Sekondari, Mwanjala Godfrey, alisema idadi na mahudhurio ya wanafunzi baada ya likizo imekuwa nzuri, lakini kuna changamoto za wanafunzi wachache ambao bado hawajaonekana na wanafuatilia kwa ukaribu wazazi na wanafunzi hao kubaini tatizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Linno Mwageni, alisema ili kukabiliana na changamoto za kielimu baada ya kufungua shule wilayani hapo ameshauri kufanyika vikao vya wazazi wiki ijayo katika shule kadhaa ili wazazi waweze kujionea mazingira ya watoto wao wakiwa darasani hasa kwa upande wa mrundikano wa wanafunzi darasani.

"Wakati wa likizo ilikuwa vigumu kuwaita wazazi kwenye vikao hivyo tutaitisha vikao wiki ijayo wakati wa masomo ili wazazi waone changamoto za watoto wao," alisema.

Kadhalika, alisema wilaya yake imehamaisha shule nyingi kuwa na mikakati ya kujikinga na corona hasa maji tiririka na sabuni kwa wanafunzi wake ili kuwa salama wawapo shuleni.

Habari Kubwa