Ripoti Maalum: Tahadhari wanaofanyiwa 'massage'

06Sep 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ripoti Maalum: Tahadhari wanaofanyiwa 'massage'
  • *Mtaalamu wa MOI atoa angalizo
  • *Afichua wachuaji wengi hawana...

INAAMINIKA kwamba, namna bora ya kuondoa msongo wa mawazo na uchovu wa mwilini ni kufanya 'massage', yaani kuchua kwa kugusa au kusugua kwa vidole maeneo yenye maumivu.

Massage kwa sasa ni moja ya huduma ambazo zimeshamiri maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, hususan kwenye saluni za wanaume na wanawake.

Hata hivyo, uchunguzi wa Nipashe jijini uliohusisha mahojiano na baadhi ya wanaotoa huduma hiyo, umebaini kwamba wanaopendelea zaidi kupata huduma hiyo ni wanaume kulinganishwa na wanawake.

Je, uchuaji huo ni salama kwa afya? Katika kudadisi usalama wa huduma hiyo, Nipashe ilimtafuta Mtaalamu wa Tiba Mazoezi kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Lucas Machage, ambaye aliweka wazi kuwa uchuaji unaoendelea kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji na maeneo mengine nje ya hospitali, haulengi tiba.

"Haufuati misingi inayotakiwa. Baada ya kuona vurugu hiyo kwa upande wa hospitali, hatuandiki 'massage; bali 'Soft Tissue Mutilation' (unyambuaji wa misuli) na hili linaweza kutimia tu kama mtu amejifunza utaalamu wa uchuaji mahali panapostahili," alisema.

Mtaalam huyo alibainisha kuwa zipo aina nyingi za uchuaji wa mwili zikiwamo za kutumia mikono kutoka sehemu moja ya mwili kwenda nyingine, uchuaji wa kukunja ngozi na uchuaji wa kutumia mikono ikiambatana na mtetemeko fulani.

“Kumbe kuna lengo kwenye kuchua na yapo mambo ya kuzingatia kitaalamu ili kupata matokeo. Matokeo hayo lazima ufuate muundo wa mwanadamu alivyoumbwa.

“Kila msuli kwenye mwili wa mwanadamu umewekwa kwenye nyumba yake, hakuna msuli uliokaa mahali ambako siyo pake, msuli unapofanya kazi unahama sehemu yake," alisema.

Machage alifafanua hoja yake, akieleza kuwa mtu anaponyanyua mikono yake juu, misuli yake inakuwa imehama eneo lake inapopaswa kuwa kama hajishughulishi na jambo lolote.

MAKOSA YA UCHUAJI

“Mtu akiwa anachua akiwa amelala kitandani, anatakiwa ahakikishe viungo vya mwili wake vinakaa kama vile Mungu alivyoviumba," anasema na kufafanua zaidi kwamba:

"Ukiweka mikono juu ya kichwa, tayari umehamisha msuli eneo lake, ukimchua katika hali hiyo, unakuwa unakandamiza misuli katika mabonde ambayo siyo yake."

Alisema kwa kufanya hivyo utamsababishia maumivu mhusika na hatapata matokeo ya kile alichokuwa amekilenga, hivyo kutotatua tatizo alilonalo.

“Unapomchua mtu kwa kulenga tiba, lazima uzingatie uumbaji wa mwanadamu. Binadamu anaanza kichwa hadi miguu.

Wakati unamchua lazima ufuate mtiririko huo, lazima utoke chini kwenye miguu kwenda juu kichwani na siyo kichwani kuja miguuni.

"Kama mtu anataka kuchua kuanzia kiunoni kwenda miguuni, mchuaji anatakiwa kuanzia miguu ili apeleke maji kwenye moyo na uchuaji wa mkono unatakiwa kuanzia kwenye vidole kwenda kwenye bega na wale wa mgongo anatakiwa kuanzia kiunoni kwenda juu," alielekeza.

Alionya kuwa endapo wachuaji wakifanya tofauti na uumbaji wa mwanadamu, madhara yake ni pamoja na kuhamisha misuli kwenye eneo lake na kusababisha maumivu kwa mhusika.

Vilevile, alisema mchuaji anatakiwa wakati akichua, asitumie nguvu nyingi bali aanze na mkandamizo mdogo na akibaini mhusika akikunja uso, anatakiwa kupunguza.

MUDA WA KUCHUA

Mtaalamu huyo alibainisha kuwa, kitaalamu muda wa ni dakika 30 na ili mtu apate matokeo chanya, lazima uchuaji uwe mwepesi na ufuate misingi ya mhusika kulala katika utaratibu sahihi, kuchua kutoka chini kwenda juu, mkandamizo mdogo na matumizi ya vidole au kiganja kulingana na eneo.

Akizungumzia hatari ya magonjwa ya kuambukiza wakati wa kuchua, mtalaamu huyo alidokeza kuwa uchuaji wa 'massage' zinafanywa na kusababisha msisimko wa maeneo mengine ambayo siyo lengo la uchuaji.

“Ndiyo maana ninasema uchuaji wa mtaani unafanywa mpaka kwenye maeneo ya siri wakidai ni uchuaji, mwisho wa siku unaweza kuleta athari nyingine za kiafya kama maambukizi ya magonjwa,” alionya.

Alibainisha kuwa ipo hatari ya kuambukizana magonjwa ikiwa anayefanyiwa ana vidonda au vipele na mfanyaji ana mchubuko kwenye kiganja.

"Uchuaji wa tiba ni lazima mtu afanyiwe vipimo baada ya mtaalamu wa afya kusikiliza historia ya mtu na maeneo anayolalamika kuchua kwa sababu unaweza kumsababishia mtu matatizo ya kiafya.

“Viungo vya mwili vinaweza kuuma, labda mtu ana malaria au ana shida nyingine mwilini, mtu wa namna hii hahitaji tiba ya kuchua,” alisema.

Mtaalamu huyo wa MOI alisema mchuaji lazima ajue eneo husika lenye tatizo na vitu gani atatumika ili kuleta matokeo chanya na siyo kuchua kwa hisia kwa kumsikiliza tu mteja.

“Huwezi kumchua mtu mahali ambako amevunjika, kuna vidonda, uvimbe au mtu ameumia leo halafu kesho akachuliwa au mgongo uliangukiwa na kitu halafu ukamchua.

Kuchua kunafanyika kwenye tatizo sugu, lakini tu kama hakuna uvimbe," alionya.

Alifafanua kuwa kuchua eneo lenye uvimbe, kunasababisha kuleta maji mengi na kusababisha uvimbe husika uongezeke.

“Kuchua kwa tiba mtu anaweza kufanya mara 12 kwa mwezi inatosha au mara tatu kwa wiki, ukishindwa hivyo unaweza kufanya kwa kufululiza na baadaye ukapunguza mara tatu au mara moja na ukamaliza,” alisema.

Alitaja njia nyingine ya kuchua ni ya kumwekea mhusika mfuko wa maji ya moto eneo husika kwa muda wa dakika kati ya 10 na 15 na baadaye akapakwa mafuta maalum ya maumivu.

“Ushauri wetu kwa wale wanaotaka huduma ya kuchua wawaone kwanza wataalamu wa tiba ya mazoezi, ili wawakague kama shida zao zinahitaji kuchuliwa au la na ni wakati gani wafanyiwe huduma hii.

“Kuna matatizo mengine hayahitaji kuchua wala kuwekewa maji ya moto, unaweza kuweka barafu tu na kupona kwa sababu tatizo ni la muda mfupi siyo la muda mrefu,” alisema.

Mtaalamu huyo pia aliwashauri watoa huduma hiyo mtaani kuvaa glovu ili kutoambukizana magonjwa.

WATOA HUDUMA

Katika udadisi wake, Nipashe ilizungumza na mfanyakazi wa saluni ya kiume ya Nevada iliyoko Sinza jijini Dar es Salaam, Angel Lyimo, ambaye alibainisha kuwa wamekuwa wakipokea wateja wengi na akakiri kuwapo kwa dosari katika kujua hali za afya zao.

“Wapo wanaokuja wakiwa na vipele au chunusi usoni au mwilini na shughuli zetu za saluni zinahusu ngozi, hivyo usipokuwa makini unaweza kuingia kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya ngozi au yatokanayo na mchubuko kama Ukimwi.

"Vifaa vinavyotumika kunyolea unaweza ukakishika vibaya kikakukata, nikipata jeraha, nisiendelee na kazi? Hapana, tunachofanya ni kuchukua tahadhari kubwa ikiwa ni pamoja na kumweleza ukweli mteja," alisema.

Lyimo alisema tahadhari wanazochukua siyo tu kwa mteja ambaye anaonyesha ana harara mwilini au chunusi, bali wakati wote hukikisha wanajali afya zao na za mteja wanayemhudumia.

“Binafsi, bado ni binti mdogo mwenye majukumu ndiyo maana nipo hapa. Siwezi kuhatarisha maisha yangu, ninachukua tahadhari. Hii ni kwa upande wa mteja anayefika hapa kutaka kufanyiwa 'scrub' (kusugua) ambayo inahitaji umsugue eneo husika kuondoa uchafu mwilini," alisema.

Mfanyakazi kazi huyo wa saluni alisema mteja anayetaka huduma ya kusuguliwa uso au mwili, kama atakuwa na chunusi mara nyingi hupewa ushauri tu wa aina ya vipodozi vya kutumia ili kuondoa tatizo na huwa hawamsugui.

“Ila ipo njia ya pili ya kutumia kifaa maalum cha kufukiza ambacho mteja mwenye chunusi badala ya kusugua kwa mkono atapakwa vipodozi vya kuondoa uchafu na kuwekwa kwenye kifaa hicho,” alisema.

Kuhusu elimu ya kuchua, Lyimo alisema alijifunza kutoka kwa mtu mtaalamu wa kutoa huduma hiyo aliyeko Magomeni na sasa ana miaka saba na hajawahi kupata malalamiko ya mteja kuwa amepata tatizo la kiafya.

“Tatizo kubwa kwenye kazi yangu, mimi ni msichana na wateja wengi wanaokuja hapa ni wanaume wa rika tofauti na unaweza kufanya kazi yako vizuri, lakini akakutaka kimapenzi.

“Na ukumbuke huduma hii mnaifanyia kwenye chumba maalum ila nikikutana na kitu hiki, ninajaribu kumwelimisha mteja kwa sababu kazi yangu ninaipenda. Wapo ambao wanaingia kwenye kishawishi na kutembea na wateja na hapo hujui afya yake kwa ujumla," alionya.

Yasini Mwinyi, mfanyakazi wa saluni ya kiume ya Family iliyoko Sinza Mori jijini, alisema wanapomwona mteja ana fangasi za miguu au chunusi usoni, huchukua tahadhari kwa kumhudumia kwa kutumia vifaa vipya kwa gharama yake.

“Tunaponunua vifaa hivyo vitatumika kwa ajili ya mteja husika. Kwa ujumla, baadhi ya huduma mfano 'pedicure' vifaa vyake tunapenda mteja anunue, vifaa ni Sh. 10,000 na huduma yenyewe ni Sh. 15,000,” alibainisha.

Kuhusu huduma za kuchua mwili, Mwinyi alisema hutozwa kwa saa, kila dakika moja ni Sh. 1,000 na hufanywa kwa ngozi ambayo ni rafiki, kwa maana kwamba haina tatizo.

“Wanaofanya kazi ya kuchua wana elimu ya kujua ni maeneo gani yanatakiwa kuguswa na ambayo hayatakiwi, kwa sababu kwenye mwili wa binadamu kuna mishipa ambayo haitakiwi kuguswa, kama siyo mtaalamu unaweza kuuvunja na kumsababishia ulemavu,” alisema.

Mwinyi alisema wanajilinda dhidi ya maradhi ya kuambukiza kwa kutoa ushauri kwa wateja ambao wanawaona ngozi zao siyo rafiki kufanyiwa huduma hiyo.

Habari Kubwa