Ruge vilio kila kona

28Feb 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ruge vilio kila kona

NI kilio kila kona ya nchi. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na namna maelfu ya wananchi wanavyoomboleza kifo cha aliyekuwa mtayarishaji wa vipindi wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (wa pili kulia), wakimfariji mama mzazi wa marehemu Ruge Mutahaba (picha ndogo), Christiana Mutahaba, wakati walipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mikocheni, jijini Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kutoa pole kwa familia. PICHA: OWM

Wakati taarifa ya familia ikieleza kuwa mwili wa Ruge unatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam kesho ukitoka Afrika Kusini na kuagwa keshokutwa, viongozi, wasanii, ndugu, jamaa na marafiki jana walimiminika kwa wingi nyumbani kwa baba yake, Mikocheni jijini, kwa ajili ya kutoa pole.

Tangu kutangazwa kifo cha Ruge juzi saa 1:40 usiku, maelfu ya Watanzania walianza kutumia mitandao ya kijamii kuomboleza huku wengi wakiandika namna alivyogusa maisha ya watu wengi hasa wasanii wa muziki wa kizazi kipya 'Bongo Fleva'.

Mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook, Twitter na Instagram tangu juzi usiku hadi jana jioni ilitawaliwa na ujumbe mbalimbali wa maombolezo ya kuhusu kifo cha Ruge, wengi wakitoa pole kwa familia na Watanzania kutokana na alivyosaidia kuinua maendeleo ya vijana wengi.

Muda mfupi baada ya umauti kumpata Ruge, Rais John Magufuli aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho, akieleza kuwa atamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, naye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa:

"Ruge Mutahaba! Tumefanya mengi pamoja kwenye afya na tulipanga kufanya mengi zaidi ili kutatua changamoto za jamii hasa kuhusu afya kwa vijana hususan wasichana balehe! Mbona umekwenda mapema? Pole zangu kwa familia, ndugu na marafiki kwa pigo hili kubwa, R.I.P Ruge".

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangallah akimwelezea Ruge kwenye ukurasa wake wa Twitter alioambatanisha na picha waliyopiga pamoja alisema:

"Ruge. Picha hii tulipiga siku moja kabla ya ajali yangu 2018. Ulikuja kuwasilisha Brand Slogan ya #TanzaniaUnforgettable kwa wadau. Bro umepigana vita vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza".

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, katika ukurasa wake wa Twitter pia alisema: "Tasnia ya habari imeshtushwa na habari za kuondoka kwako ghafla, umeacha pengo ambalo ni gumu kuliziba. Ulikuwa mtu muungwana kweli kweli na mtu mahiri kwenye tasnia ya habari, nenda salama kaka yetu. "Pumzika kwa amani Ruge.

Wakati umekaa nyumbani kwa Mungu Baba, usisahau taaluma yako. Najua na ninaamini wewe ni mbunifu wa hali ya juu, nina uhakika utatafuta njia ya kuwasiliana nasi. Poleni sana familia ya Ruge Mutahaba, wanahabari na Watanzania wote."

Mapema jana asubuhi, Nipashe iliweka kambi nyumbani kwa baba wa marehemu Ruge Mikocheni jijini na kushuhudia namna mamia ya watu walivyokuwa wakifurika kuomboleza.

Viongozi mbalimbali walioko madarakani na wastaafu walikuwa wakipishana kwenye geti la kuingia kwenye msiba huo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari na barabara kuu kufungwa kwa muda kuruhusu viongozi hao kupita.

WAZIRI MKUU MSIBANI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwasili msibani jana mchana na kutoa salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Magufuli mbele ya umati wa waombolezaji waliokuwa msibani.

Majaliwa alisema taifa limepoteza kijana aliyekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha vijana wajitambue, wawe wazalendo kwa nchi yao na watambue fursa za maendeleo zilizopo badala ya kuwa walalamikaji.

Majaliwa alisema vijana nchini walikuwa na kiongozi aliyekuwa akiwaongoza kwa kuwafungua kimawazo na kuwaonyesha fursa mbalimbali zitakazowawezesha kuwakwamua kifikra na kiuchumi ili kujitegemea.

Alisema msiba huo ni wa wote kwa kuwa Ruge alifanya kazi kubwa ya kushirikiana na serikali kuhamasisha vijana kujitambua na kutambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi.

Waziri Mkuu alisem Ruge katika uhai wake, amefanya kazi kubwa kwa serikali, kuanzia awamu ya nne hadi ya tano hususani katika kuhamasisha vijana kujikwamua na kuacha utegemezi.

Majaliwa alisema historia ya Ruge inaeleza namna alivyozunguka nchi nzima na kukutana na makundi mbalimbali ya vijana na kuwaelimisha namna ya kutambua fursa zilizopo huku akiwahamasisha kuwa wazalendo.

"Marehemu alikuwa akitoa hadi fedha zake binafsi kwa ajili ya kuwawezesha vijana hasa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kiuchumi ili nao washiriki katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na hatimaye waondokane na utegemezi," alisema.

Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), alisema Ruge alikuwa kijana mwenye kipaji cha pekee ambaye atakumbukwa kwa ubunifu wake wa mawazo yaliyotoa fursa kwa vijana ndani na nje ya nchi.

Nchemba alisema maisha ya Ruge yalikuwa elimu tosha kwa vijana wanaopenda kutumia fursa zilizopo kubadilisha maisha. "Mara ya kwanza nilipokutana naye, nilikuwa mweka hazina wa chama na alinishauri namna tunavyoweza kutumia rasilimali zetu nyingi ambazo zimelala zikaenda kwenye maisha yetu. Miaka miwili iliyopita, anishauri kwamba jimboni kwangu lazima nibuni kitu ambacho baada ya muda wananchi wangu watakuwa wananitambulisha kupitia kitu hicho," alisema.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alimwelezea Ruge kuwa ni kijana mbunifu ambaye ameshiriki kwa kiasi kikubwa kukuza vijana wenzake na kuwa kiunganishi.

"Neno langu fupi sana ni kwamba tumepoteza mtu muhimu sana, lazima tusikitike, lazima tulie lakini pia lazima tusherehekee maisha yake. Ruge ameishi maisha ambayo ameacha alama," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile, alisema kifo cha Ruge ni pigo kubwa kwa sababu taifa limempoteza mtu ambaye aliwafundisha vijana kutambua fursa zinazowazunguka.

Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema Ruge alikuwa zaidi ya jina lake kwenye chombo cha habari kilichoajiri watu wengi kwa kuwa alijitoa kuhakikisha vipaji vinageuzwa kuwa fursa.

Mbali na Waziri Mkuu, viongozi wengine waliofika kwenye msiba huo jana ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, wakuu wa wilaya, wabunge na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

KUAGWA JUMAMOSI

Akitoa ratiba ya awali jana mchana baada ya kikao cha familia, msemaji wa familia, Annick Kashasha, alisema mwili wa Ruge unatarajia kuwasili Tanzania kesho ukitoka Afrika Kusini alikokuwa amelazwa tangu mwaka jana kwa matibabu ya figo.

Alisema endapo mambo yatakwenda kama ratiba ilivyopangwa, mwili wa Ruge utazikwa Jumatatu katika Kijiji cha Kiziru, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Kashasha alisema zipo changamoto zilizojitokeza Afrika Kusini ambazo kama zitatatuliwa kwa wakati kwa mujibu wa ratiba yao, mwili wa marehemu Ruge utawasili kesho na kusafirishwa Jumapili kuelekea kijijini kwao Kiziru kwa ajili ya mazishi.

"Ndugu na jamaa walioko Afrika Kusini wanaendelea kufanya jitihada zote za kuhakikisha mwili wa Ruge unarejeshwa Tanzania. Zipo changamoto zilizojitokeza ambazo walioko kule wanazifanyia kazi, wakiweza kuzitatua, mwili utarejeshwa nchini siku ya Ijumaa (kesho)," alisema.

"Iwapo mwili utafika Ijumaa, ina maana taratibu za kuaga mwili zitafanyika Jumamosi hii na mwili utasafirishwa kwenda Bukoba siku ya Jumapili. Huu ndiyo uamuzi wa famili, kwamba Ruge atazikwa Kijiji cha Kiziku, Bukoba mkoani Kagera. Hii ndiyo ratiba ya awali ambayo imetokana na kikao tulichokaa, kama kutakuwa na mabadiliko, tutajulishana."

DUDU BAYA MATATANI

Wakati huo huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe, ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kumchukulia hatua kali na za kinidhamu msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Dudu Baya, kwa kejeli alizozitoa kwa marehemu Ruge Mutahaba.

*Imeandaliwa na Romana Mallya na Beatrice Shayo

Habari Kubwa