Samia aahidi kutenda haki CCM

01May 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Samia aahidi kutenda haki CCM

RAIS Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akiahidi kuendeleza mfumo thabiti wa uwazi, kutoa haki katika michakato ya uchaguzi wa ndani ya chama na wa kuwapata wawakilishi katika nafasi za kitaifa.

Mbali na hilo, ameahidi kusimamia misingi ya chama, kuendeleza utamaduni wa kujitathmini, kujisahihisha na kufanya mabadiliko kwa lengo la kukiimarisha chama.

Kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 1,876 jana, Rais Samia alichaguliwa kwa kishindo kwa kupata kura zote 1,862 za wajumbe 1,862 waliopiga kura.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Samia alisema anakwenda kujenga imani kwa wananchi na kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea duniani.

"Ninajua jukumu mlilonipa la kuwa mwenyekiti siyo rahisi, ila nitaweza, sababu za kwaza ni kwamba CCM inaongozwa na kanuni, taratibu na katiba ambayo ninaahidi nitaifuata.

 

“Nimekuwa mwanachama wa CCM kwa miaka 34, nina uzoefu wa miaka 20 ndani ya vikao vikubwa vya kufanya uamuzi. Ninayajua yanayoamuliwa ndani ya chama. Ninajua ndani ya CCM kuna umoja, ushirikiano na mshikamano," aliahidi.

Rais Samia pia aliahidi kujikita katika kuwahamasisha viongozi wenzake katika ngazi zote ndani ya chama kupitia kwa kina sera na miongozo inayoelekeza itikadi, imani, mwelekeo na majukumu ya chama.

Alisema lengo kuu ni kuangalia masuala yanayofaa kwa hali na mwenendo wa dunia kwa wakati wa sasa kwa lengo la kusonga mbele.

“Pia nitasimamia maadili, kanuni za chama ili kujenga misingi ya wanachama wanaotambua wajibu wao kwa chama na taifa lao," alisisistiza.

Habari Kubwa