Samia ahutubia Bunge la Kenya

05May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Samia ahutubia Bunge la Kenya

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara yake nchini Kenya sio ya bahati mbaya bali imelenga kukazia maeneo yaliyolegalega katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Akihutubia Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti Rais Samia, ametaja mafundo matatu ambayo yanafanya uhusiano wa Kenya na Tanzania kuwa wa lazima na siyo hiyari.

Akitaja mafundo hayo Rais Samia alisema fundo la kwanza ni undugu wa kibinadamu kati ya wananchi pande zote mbili ambao hauwezi kutenganishwa na mipaka ya kuchorwa kwenye ramani, makabila ya pande mbili za mpaka wanaingiliana na watu wake ni wale wale wamoja.

“Tanzania ina pakana na nchi nane, lakini nchi ya Kenya pekee ndio tunajamii nyingi zilizoko katika pande mbili za nchi zetu, kwenye ukumbi huu wa bunge kuna akina Otieno, Bohke, Namelok, kama ilivyo Tanzania.

“Lakini pia kuna wakina Kilonzo na Kihoko kama ilivyo Tanzania, lakini zaidi kuna Mohamed Fakhi Mwinyi Haji, huyu ni Seneta wa Mombasa, lakini hili ni jina safi la Kizanzibari kwa hiyo hatuwezi kutengana.” alisema.

Alitaja fundo la pili ni historia ambayo kabla ya kuanzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwaka 1967, nchi hizo mbili za Tanzania na Kenya tayari zilishakuwa chini ya Mamlaka ya Huduma za Pamoja za Afrika Mashariki (EACSO) ambapo huduma muhimu ikiwemo uchumi zilifungwa pamoja kabla ya nchi hizo kupata Uhuru.

Rais Samia alitaja fundo la tatu kuwa ni Jiographia ya nchi hizo mbili ambazo ni rahisi kufikika na pia zimejaliwa rasilimali muhimu ikiwemo bahari na hardhi.

“Ikolojia yetu ni moja tuna maumbile ya asili ambayo hatuwezi kuyatenganisha, lakini hata wanyama wetu ni ndugu, na ni majirani, kuna wale wanyama pori wanakuja kupata mimba Kenya wanazalia Tanzania, sasa ingekuwa wanyama wana uraia wangekuwa raia wa wapi?” alihoji Rais Samia na kuongeza

“Wanyama wakitoka Serengeti wanaingia Masaimara, lakini siku hizi hata Tausi wetu waliopo Ikulu ya Tanzania wana ndugu zao Ikulu ya Nairobi kwa hiyo kama Tausi na wanyama wana undugu, sisi wanadamu tunatengana wapi?.....; “

Hatuna sababu ya kutengana, kutokana na ukweli huu ushirikiano wetu sio wa hiyari ni lazima, kutokana na kanuni ya uasili, undugu, ushirika na ujirani yote wanatufanye tuwe wamoja.

“Ushirikiano wetu sio wa hiyari ni wa lazima, ili la maumbile hatuna la kubadilisha ama tupendane au tuchukiane, ama tucheke au tununiane, kwa kila hali, iwe heri au dhiki, tunategemeana, panapotokea ukame Tanzania, njaa inabisha hodi Kenya, panapokosekana uzalishaji Kenya, bidhaa zinakosekana Tanzania, hivyo tupatane na tufanye kazi pamoja.

Rais Samia amesema anashangaa sana watu wanaosema eti Kenya na Tanzania ni washindani, eti uhusiano wao ni wa kukamiana na kwamba anawashangaa wanaodhani kuwa Kenya au Tanzania inaweza kusimama peke yake, na kwamba wanaodhani hivyo ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu.

“Watu hawa wapo pande zote na hata wanasiasa wa pande zote bahati nzuri tu ni kwamba sio wengi ndio maana uhusiano wetu unatimiza miaka 56 sasa ya kiseriakali.

Habari Kubwa