Samia akoleza moto ajira SADC

06Mar 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Samia akoleza moto ajira SADC

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka mawaziri wa sekta ya kazi na ajira wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupambana na tatizo la ajira kwa vijana kwa kuweka mikakati thabiti.

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, picha mtandao

Vilevile amewataka kuweka uwiano sawa kati ya matumizi ya nguvu kazi na teknolojia ili kuhakikisha vijana wa SADC wanaendelea kunufaika na fursa za ajira zinazozalishwa katika nchi zao.

Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa mawaziri wa sekta ya kazi na ajira na wadau wa utatu wa SADC ambao watakutana kwa siku mbili kujadiliana masuala ya kazi, ajira na uhamaji wa nguvu kazi.

Alisema ukosefu wa ajira kwa vijana umebaki kuwa changamoto ya kidunia na kwamba taarifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu mwenendo wa soko la ajira kwa mwaka 2020, zaidi ya watu milioni 187.7 (sawa na asilimia 5.5) duniani hawana kazi.

Aliongeza kuwa takribani wafanyakazi Sh. bilioni mbili (sawa na asilimia 61.12) wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi na zaidi ya watu milioni 267 (sawa na asilimia 22) wenye umri kati ya miaka 15 na 24 hawako kwenye mafunzo wala katika ajira.

“Ni vijana milioni 429 (sawa na asilimia 36) tu ndio walioko kwenye mafunzo na walioko katika ajira ni milioni 509 (sawa na asilimia 42). Hii ni changamoto kubwa ambayo sisi SADC kama sehemu ya dunia, inatuhusu na tunalazimika kuweka mikakati ya kupambana nayo,” alisema Samia.

Aliongeza kuwa maendeleo ya nchi yoyote huletwa na nguvu kazi ya vijana na kwamba kwa wastani inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi katika SADC ni vijana.

“Kwa mantiki hiyo, hatuna budi kuitumia nguvu kazi hii ipasavyo ikizingatiwa kuwa yapo mahusiano makubwa kati ya nguvu kazi hiyo na ukuaji wa uchumi wa nchi zetu na kuondoa umaskini,” alisema.

Samia alisema mtu akipata ajira, hupunguza kiwango cha umaskini kwa njia mbalimbali, hivyo SADC haina budi kuwekeza katika kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki vizuri na kwa tija katika ukuzaji wa uchumi wa nchi wanachama.

Kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, Samia aliwataka viongozi wa SADC kulitengenezea mikakati mizuri itakayowezesha wananchi wa jumuiya kunufaika.

“Uhamaji wa nguvukazi umekuwa na matokeo chanya na hasi katika nchi za Sadc, matokeo chanya ni pale ambapo nchi zetu zinanufaika na uendelezaji wa ujuzi wa nguvu kazi kutoka nchi za nje au zinazoendelea,” alisema Samia.

Aidha, Samia aliwataka wakuu hao kufikia maamuzi yaliyo sahihi na kuona ni kwa namna gani Sadc itawezesha nguvu kazi inayohama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kupata fursa za ajira zenye staha pamoja na kuwezesha uhamishaji wa mafao ya hifadhi ya jamii.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema mawaziri hao watakuwa na majadiliano ya siku mbili kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo mikakati ya kisera kuhusu kazi na ajira.

Alisema uwapo wa fursa za ajira katika ukanda wa Sadc kutakuza maendeleo, uchumi wa viwanda pamoja na kuondoa umaskini.

Habari Kubwa