Samia amulika maadili vijana

03Oct 2021
Augusta Njoji
DODODMA
Nipashe Jumapili
Samia amulika maadili vijana

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema licha ya uwapo kwa mifumo ya kuwajenga vijana kimaadili, bado kuna idadi kubwa ya wanaopotoka nchini.

Alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya Siku ya Mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Rais alikitaka Chama cha Skauti, Girl Guides na Umoja wa Vijana wa vyama mbalimbali vya siasa kujiuliza wanapokwama kutokana na kuwa na idadi kubwa ya vijana ambao wana ukosefu wa maadili.

"Ukiangalia mfumo wa Skauti, wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umoja wa vijana wa vyama vingine vya siasa, Girl Guides wetu, ukosefu wa maadili unatoka wapi Tanzania ikiwa tuna taasisi zote hizi zenye mifumo mikubwa ya kulea vijana lakini bado tuna idadi kubwa ya vijana wanaopotoka?

"Tujiulize tumekwama wapi, tumekosea wapi na hilo swali naliacha kwa taasisi zote nilizozitaja hapa, tujiulize tunakwama wapi, kwa nini vijana wetu wapotoke wakati tuna mifumo yote hii?" Rais alihoji.

Alisema mfumo wa Skauti ni mkubwa na unaendana na serikali na kuahidi kuimarisha zaidi chama hicho ambacho kinawaunganisha vijana bila kujali dini, kabila, rangi au itikadi ya vyama vya siasa.

Rais Samia alibainisha kuwa chama hicho ni muhimu katika kuwalea vijana kwenye maadili mema, ukakamavu na kuwaandaa viongozi wajao wa taifa.

"Umuhimu huu wa Skauti umeongezeka zaidi katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, endapo hatutawaandaa vijana wetu, upo uwezekano mkubwa wa kurubuniwa na kuangukia kwenye vitendo au makundi maovu," alitahadharisha.

Rais Samia aliongeza: "Baraza la Skauti liendelee kuwafundisha kiapo na kanuni hizi watoto wetu wanapojiunga, mjitahidi kuwachukua wakiwa na umri mdogo, tukiweza kuwafundisha kwa watoto wadogo jambo hili litakaa, Skauti wengi wakiingia kwenye ajira zao huwezi kuta wanahujumu, kuiba au kufanya kinyume cha maadili."

Aliwataka Skauti wa Tanzania kuishi kwa kiapo na vitendo na kuwa mfano kwa jamii ili kuhamasisha wengine kujiunga.

Hata hivyo, Rais Samia aliwataka kubeba ujumbe wa  kuhamasisha na kuelimisha watu kubadili mawazo yao na kuwa na hiari ya kuchanjwa ili kujikinga na vifo na ukali wa maradhi ya corona.

"Lingine, mwakani nchi yetu itaingia kwenye kuhesabu watu, watanzania tujuane tupo wangapi kwenye maeneo yapi, zoezi litaingia makazi ya Watanzania, tuna majumba mangapi ya aina gani, yapo wapi? Tutaweka mipaka kwenye vitongoji na vijiji na kujiepusha na migogoro inayokuja wakati wa uchaguzi wetu.

"Pia sensa inaenda kutusaidia kuweka anuani baada ya kujua makazi, tunaomba Skauti msaidie na ikibidi mjitoe kwenda kusaidia zoezi hili liende vizuri," alisema.

Kuhusu uhaba wa fedha za kuendesha shughuli za Skauti, Rais Samia alikipongeza chama hicho kwa kubuni na kutafuta suluhisho la kero kwa kuweka vitega uchumi ambavyo vitatumika kuinua uchumi wao na kuahidi kuwaunga mkono.

"Kuhusu kuirudisha Skauti kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu, jambo ambalo sitaki kuahidi hapa tutalifanyia kazi, tukiingiza kwenye wizara, Girl Guides watakuja waingizwe, vyama vingine watakuja waingizwe, nitakachofanya ni kuangalia mbinu za kusaidia kufanya kazi yenu lakini sio kuwarudisha.

"Nafasi za uteuzi mfano mzuri RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) wa Kigoma yupo hapa, bila shaka kuna Skauti wengi wameteuliwa lakini hawajavaa sare lakini tumechukua tutazingatia, ila wanapojaza CV (wasifu) hawasemi kama ni Skauti, wanaandika sifa za shule, unajikuta unateua Skauti hujui kama ni Skauti," alisema.

Awali, Skauti Mkuu wa Tanzania, Mwamtumu Mahiza, alisema zaidi ya Sh. bilioni 34 zinahitajika kulipa fidia, kujenga majengo na vifaa vya kujifunzia kwenye jengo litakalojengwa Dodoma.

"Ninakuomba Rais ambaye ndiye Mlezi wa Skauti kuwezesha kupata fedha hizo ili mradi huo uanze na chama kijitegemee," alisema.

Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, alisema Serikali ya Zanzibar ipo kwenye mchakato wa kuwapatia eneo la Kijiji cha Skauti.

Habari Kubwa