Samia:Sitabagua wenye weledi,umahiri

07May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Samia:Sitabagua wenye weledi,umahiri

RAIS Samia Suluhu amesema katika kuimarisha uchumi hatabagua mtanzania yeyote mwenye weledi na umahiri anayeweza kuleta manufaa kwa Taifa hata ikibidi kutoka chama kingine cha siasa tofauti na chama chake .

Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Mlimani City ambapo amewaambia wazee hao wasishangae pale watakapomuona anafanya mabadiliko hata kama yatawagusa vijana wao.

“Katika kupanga safu za kujenga uchumi sitochagua, mtanzania yeyote mwenye weledi na umahiri anayeweza kuleta manufaa kwa Taifa nitamuingiza afanye kazi, sitochagua huyu katoka chama kipi yule katoka chama gani, lengo letu ni kujenga umoja wa watanzania'' - Rais Samia Suluhu.

"Niwaombe Wazee wangu wa Dar es Salaam tumedhamiria kwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu ya uongozi niwaombe tu pale mtakapoona mabadiliko hayo yamewagusa watoto wenu au ndugu zenu msikasirike ni kwa nia njema tu “ amesema Rais Samia.

Kuhusu wazee kulipwa pensheni kama walivyoomba Rais Samia amesema suala hilo kwa sasa bado gumu hadi pale uchumi wa nchi utakapokaa vizuri baada ya kuharibiwa vibaya na janga la Corona.

Kuhusu ulinzi na usalama Rais Samia ameonya tabia ya wizi iliyoanza kuibuka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam na kulitaka jeshi la polisi nchini kuchukua hatua kukomesha hilo.

 

 

 

Habari Kubwa