Serikali yaunda jopo uchunguzi aliyeanguka mtini akisaka fimbo

17Dec 2018
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yaunda jopo uchunguzi aliyeanguka mtini akisaka fimbo

SERIKALI imeunda kamati kuchunguza tukio la mwanafunzi Amos Gabriel, aliyepata ulemavu wakati akitafuta fimbo shuleni jijini Mbeya miezi minane iliyopita.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Samora Machel, anadaiwa kuanguka alipopanda mtini kusaka fimbo aliyotumwa na mwalimu wake.

Inadaiwa mwanafunzi huyo baada ya kutumwa kufuata fimbo na mwalimu wake alikosa na kulazimika apande mtini.

Inadaiwa kuwa akiwa juu ya mti, alianguka na kuteguka shingo, kuvunjika mikono na kupata matatizo kwenye uti wa mgongo, ajali ambayo imesababisha kushindwa kutembea.

Mbali na kuunda kamati hiyo, serikali imeahidi kusaidia matibabu ya mwanafunzi huyo ili afikie ndoto yake ya kuwa daktari bingwa, ikikabidhi Sh. milion 9.46 jana kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.

Akizungumza na Nipashe jana, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, alisema tayari ofisi imeshatoa maelekezo kwa uongozi wa Mkoa Mbeya iundwe kamati kujiridhisha na suala hilo.

Alisema kuwa pia wameuagiza uongozi wa mkoa huo kuhakikisha unasimamia matibabu ya mwanafunzi huo.

"Tukio hilo limeonekana kwenye mitandao ya kijamii na limewagusa watu wengi, naomba jambo hili tuchukulie kama ajali nyingine lisiwe na tafsiri nyingine," Waitara alisema.

"Sisi kama serikali tupo pamoja na mwanafunzi huyu ili kuhakikisha anafikia ndoto yake aliyosema ya kuwa daktari bingwa."

Waitara aliwashukuru maofisa elimu ngazi ya taifa, mkoa na halmashauri ambao baada ya kuona changamoto hiyo, waliguswa na kuamua kuchanga Sh. milioni 9.46 zilizokabidhiwa.

"Tunajua anaendelea na matibabu na gharama ni kubwa, tunaomba wadau na Watanzania wengine tuungane kwa pamoja kumsaidia mtoto huyu," alisema.

Waitara alisema fedha hizo tayari zimeshawekwa kwenye akaunti 0152413629000 ya mwanafunzi huyo iliyoko CRDB.

"Hatuwezi kujua huenda Mungu alikuwa na mpango wake atasaidiwa matatibu, lakini tumeshatoa maelekezo atafutiwe shule ya karibu aendelee na masomo yake," alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, Tixon Nzunda, alisema serikali iliona tukio hilo katika mitandao ya kijamii na kuamua kumtafuta na kutoa pole kwa familia.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Felix Lyaniva, alisema amepata taarifa kwa mama mzazi wa mtoto huyo kuwa anatumia Sh. 40,000 kulipa gharama za usafiri wa kumpeleka hospitali.

Kutokana na changamoto hiyo, Lyaniva alisema atatoa gari litakalokuwa linatumika kumpeleka hospitali kila anapokuwa anatakiwa kwenda ili kuipunguzia gharama familia.

"Ninashukuru serikali kwa huu msaada, kikubwa naomba mwanangu apate matibabu ya zaidi ili arudi katika hali yake na aendelee na masomo yake maana hicho ndicho amekuwa akinisumbua, utakuta ananiambia nipeleke shule hivihivi nilivyo," alisema Swaumu Ramadhani, mama mzazi wa mwanafunzi huyo.

Gabriel aliwashukuru viongozi hao wa serikali kwa msaada wao, lakini akaomba asaidiwe zaidi kupata matibabu ya kibingwa ili apone haraka na kurejea shule kuendelea na masomo yake.

"Wale wanafunzi wa Shule ya (Lucky) Vincent waliopata ajali walipelekwa nje na kupona, na mimi naamini nikipelekwa huko nitapona haraka, naomba nipatiwe msaada huo," alisema.

Habari Kubwa