Serikali kuboresha bajeti ya uvuvi

31Mar 2021
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Serikali kuboresha bajeti ya uvuvi

SERIKALI imesema kuwa katika bajeti ya sekta ya uvuvi ya mwaka 2021/22 imepanga kuboresha shughuli za uvuvi wa bahari kuu nchini na inatarajia kuanza ujenzi wa bandari itakayosaidia kuongeza mapato yataokanayo na mazao ya uvuvi.

Aidha, katika bajeti hiyo kiasi cha Sh. Bilioni 50 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ya uvuvi.

Katibu mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya uvuvi Dk. Rashid Tamatama, amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo mbele ya kamati ya bunge ya mifugo, maji na kilimo.

Amesema katika bajeti hiyo maeneo ya vipaumbele ni pamoja na ujenzi wa bandari ya uvuvi itakayo jengwa ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo nchini.

Dk. Tamatama, amesema kuwa hivi sasa mchakato wa kujenga bandari hiyo ya uvuvi upo katika hatua za kuandaaji wa michoro na mara baada ya kukamilika hatua nyingine itafuata.

“Ili kuboresha shughuli hizi za uvuvi kuwa na tija na kuongeza pato la taifa kupitia sekta hii lazima tujenge bandari ya uvuvi itakayo saidia kuongeza uvunaji wa samaki tofauti na ilivyosasa na katika bajeti yetu hii tumetenga Sh. bilioni 50, kwa ajili ya ujenzi huo” amesema Dk. Tamatama.

Pia, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa inafufua shilika la uvuvi nchini ili kusimamia shughuli za uvuvi.

Habari Kubwa