Serikali yaanza kununua mahindi

15Sep 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Serikali yaanza kununua mahindi

NEEMA imetua kwa wakulima wa mahindi baada ya serikali kuanza kununua tani 90,000 kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

Ununuzi huo umeanza baada ya serikali kutoa Sh. bilioni 50 ili kunusuru soko la mahindi ambalo lilionekana kusuasua hivi karibuni. Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, alisema NFRA itaanza kununua kwenye mikoa saba kwa bei ya Sh. 500 kwa kilo na CPB itanunua kwenye mikoa sita kulingana na bei ya soko. Waziri alitaja mikoa saba ambayo NFRA itaanza kununua mahindi hayo kuwa ni pamoja na Ruvuma, Rukwa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Iringa na CPB ikinunua mikoa ya Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe, Dodoma na Manyara. Alibainisha mwaka huu zimezalishwa tani milioni sita za mahindi huku ziada ikiwa mara mbili ya uzalishaji uliofanyika kwa mwaka uliopita huku nchi za Zimbabwe na Zambia zikitajwa kuzalisha kwa wingi nafaka hiyo. “Mwakani bei inaweza kupanda lakini kwa kuwa kuna mikoa inaongoza kwa uzalishaji nchini kama Ruvuma ukifuatiwa na Rukwa, bei ni ndogo sana wakati Mkoa wa Katavi, Songwe zikiwa chini zaidi hali inayopelekea mkulima kushindwa kupata fedha za kujikimu na kujiandaa kwa msimu ujao," alisema. Waziri huyo alisema mahindi hayo yatanunuliwa kupitia Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) au vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa na kwa wakulima wadogo kwa magunia yasiyozidi 300 au tani 30. "Tunataka rekodi ya kila mkulima aliyelima mahindi yanunuliwe na fedha zilizotolewa na serikali zitumike kama ilivyokusudiwa. "Baada ya zoezi hili kufanyika, wizara itafanya ufuatiliaji kwa viongozi wa mikoa ili kupata taarifa na namna mgawanyo wa ununuzi ulivyofanyika kwenye mikoa tajwa," alisema. Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Milton Lupa, alisema wanakwenda kununua nafaka hiyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwenye mikoa ya Ruvuma, Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa kupitia AMCOS na wakulima waliosajiliwa. "Wananchi watulie tutanunua mahindi, wapunguze vurugu kwa kuwa tutafuata utaratibu uliowekwa, tunawahakikishia tutawafikia wakulima wenye kipato cha chini wenye mahindi yanayokidhi vigezo," alisema. Mkurugenzi Mkuu CPB, Dk. Anselm Mushi, alisema watanunua mahindi hayo kama walivyoelekezwa na wizara na kwamba wameshaanza kutafuta masoko nje katika nchi za Kenya, Sudan Kusini, Comoro, Burundi na Rwanda.